WANANCHI wa vitongoji vinne katika kijiji cha Manyire kata ya Mlangarini wilayani Arumeru mkoani Arusha wameamua kujitolea kutengeneza barabara baada ya viongozi wa kata kushindwa kupeleka huduma hiyo tangu mwaka 1977.
Vitongoji vyenye changamoto hiyo pamoja na umeme ni Majengo, Olmesera, Makao Mapya na kitongioji cha Upendo.
Mbali na barabara pia wananchi hao wamesema huduma ya umeme katika vitongoji hivyo imekuwa changamoto kwao na kusema kuwa huduma hiyo wamekuwa wakiiona vitongoji jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo, Hilda Kaaya alisema nyakati za masika watoto wa shule hujipa likizo kwani hawawezi kwenda shule kwa kuhofia maji katika mito iliyosambaa katika vitongoji hivyo.
Kaaya alisema mwananchi anapopata msiba maiti hubebwa begani umbali wa zaidi ya km 15 ili aweze kupata usafiri kwenda hospitali vinginevyo hali inakuwa mbaya kwa mfiwa.
Alisema kutokana na hali hiyo wameiomba serikali ya wilaya kutupia macho katika vitongiji hivyo ili viweze kupata huduma hiyo kama vitongiji vingine.
Kiongozi huyo alimtupia lawama diwani wa kata hiyo, Zabedayo Mollel na kusema kuwa toka alipofika katika vitongiji hivyo kipindi cha kuomba kura mwaka 2020 hajawahi kufika pamoja na kupewa taarifa mara kwa mara bila mafanikio.
Mwenyekiti wa Kamati ya Barabara, Rogers Kisanga alisema kuwa amekuwa akihamashisha watu kujitolea kwa hali na mali kukarabati barabara mara kwa mara lakini imefika mahali amezidiwa kwa kuwa viongozi wa kata wamekuwa wazito kutoa ushirikiano.
Kisanga alisema na kuuomba uongozi wa serikali wilaya hususani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha kuhakikisha fedha za maendeleo ya kata zinafika katika vitongoji hivyo kwa maslahi ya wote kwani hana imani kama fedha zinafika kwa malengo yaliyokusudiwa.
‘’Tunakuomba Mkurugenzi Arusha DC tumia mamlaka yako kuhakiki fedha za maendeleo ya kata kufanya kazi inayokusudiwa kwa kuwa hawaoni kama fedha hizo zinawafikia ‘’alisema Kisanga.
Mwananchi John Mushi yeye alitoa lawama zote wa diwani Mollel kwa kuwa hana msaada kwa wananchi wa vitongoji hivyo toka alipochaguliwa.
Mushi alisema na kuutaka uongozi wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuhakikisha wanatembelea vitongiji hivyo na kusikiliza kero zinazowakabili ili waweze kuzipatia ufumbuzi.
Mwananchi mwingine, Fredrick Kisanga yeye alisema kuwa mbali ya changamoto ya barabara pia huduma ya maji katika vitongiji hivyo ina shida na kuwataka viongozi kuwajibika katika kazi na sio kukaa ofisini.
Alipopigiwa simu diwani wa kata hito Zabedayo Mollel na kuelezwa tuhuma anazotuhumiwa na wananchi wake hakujibu chochote na alikata simu na baada ya kupigiwa tena alizima simu yake ya kiganjani.
Comments are closed.