Wananchi Mtwara walivyompokea Rais Samia

BAADHI ya Wananchi mkoani Mtwara leo wamejitokeza kwa wingi uwanja wa ndege kumpokea Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wakiwa uwanjani hapo wananchi hao wamezungumza na HabariLeo namna ambavyo wanatarajia juu ya ujio huo wa Rais katika mkoa huo.

Asha Mohamed amesema wamepokea kwa furaha kubwa kwasababu ni fursa ya kuwafanya wawekezaji waweze kuja kwa wingi na kukuza uchumi kupitia uwekezaji mkubwa uliyofanywa na serikali.

‘’Tuna imani kubwa kuwa ujio wa Rais katika mkoa huu atatembelea na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo kama bandari, uwanja wa ndege na mingine kwahiyo ni fursa na heshima kubwa sana wanamtwara mh Rais kufanya ziara katika mkoa wetu.” amesema Mohamed.

Hamisi Bakari amesema wana imani kubwa na viongozi wao wote kwa ujumla kwahiyo ujio wa Rais ni fursa kwao kwasababu kuna baadhi ya vitu ambavyo vimejifunga yeye atavifungua ili uchumi wa wanamtwara uzidi kuimarika.

‘’kiukweli uchumi wa mtwara kwa sasa umekuwa mgumu sana biashara zimejifunga mfano zao la korosho kwa sasa halifanyi vizuri, maisha kwa ujumla yamekuwa magumu kwahiyo ujio wa Rais Samia tuna imani mambo mengi yatafunguka.

” amesema Bakari.

Mbunge wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe amesema Rais Samia katika ziara yake hiyo atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo  pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo wabunge hao wamefurahia ujio huo kwasababu atafungua milango zaidi ya fursa za maendeleo katika maeneo yao.

Aidha Rais Samia yuko na ziara ya siku nne mkoani humo kuanzia leo Septemba 14 mpaka Septemba 17 mwaka huu ambapo atatembelea, kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button