WAKAZI wa Kitongoji cha Ndolo, Kata ya Ndanda Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wameishuru serikali kwa kuwaletea mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndanda -Miyuyu kilometa 1.8 kiwango cha lami unaogharimu zaidi ya Sh milioni 900.
Akizungumza leo Aprili 8, 2023 Mwenge wa Uhuru ulipotembelea na kuweka Jiwe la Msingi miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Alfonce Fundi amesema ujenzi wa barabara hiyo utasaidia wananchi wa maeneo hayo na mengine kuondokana na changamoto ya barabara ya usafiri.
Amesema kabla ya mradi huo barabara ilikuwa haipitiki hususani kipindi cha mvua hivyo kusababisha wananchi wa Kitongoji hicho na kwengine kushindwa kufika kwa wakati kutoka eneo hilo kwenda jingine.
Stella Philipo mkazi wa Kitongoji hicho amesema kabla ya mradi ajali nyingi zilikuwa zikitokea kwenye barabara hiyo kutokana na kuwepo kwa mlima katika barabara hiyo lakini pia ilikuwa ikichelewa baadhi ya shughuli za maendeleo ikiwe usafirishaji wa mazao.
“Hii barabara ina mlima sasa kabla ya huu ujenzi ajali zilikuwa zinatokea hasa kipindi hiki cha mvua na mfano mgonjwa akizidiwa anachelewa kufika hospitalini kutokana na uchakavu wa barabara kwa hizo siku za nyuma”, amesema Stella.
“Kwa sasa tunaipongeza sana serikali kwa kututejengea barabara hii kwani tumeshaondokana na adha iliyokuwa ikituka bili kwa mda mrefu sasa””,Ameongeza .
Meneja wa Barabara za Vijijin na Mijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Patrick Kanyagha amesema mradi umefikia asilimia 100 kwa ujenzi wa awamu ya kwanza na asilimia 89 ujenzi wa awamu ya pili ambapo ulianza kutekelezwa Agosti 2022 na ulitarajiwa kukamilika Februari 2023.
Amesema faida ya mradi huo ikiwemo kupunguza kwa gharama za matengenezo zilizokuwa zikitumika kila mwaka, kurahisisha usafiri kufika hospitali ya rufaa ya Ndanda, ajali za barabarani kwa kiwango kikubwa lakini pia ajira kwa vikundi maalum ikiwemo mama lishe na Vijana.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim ameridhia kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo kwani umekidhi vigezo na ubora huku kuwataka wataalam wilayani humo wazingatie suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira kutokana ndiyo kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu.