Wananchi Themi waondokana na changamoto ya maji

WANANCHI zaidi 5000 wa Kata ya Themi Halmashauri ya Jiji la Arusha, mkoani Arusha wameondokana na adha ya huduma ya maji baada ya mfadhili kutoka nchini Oman kuwachimbia visima viwili vitakavyosaidia  kuondokana kero hiyo ya muda mrefu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo diwani wa kata hiyo, Lobora Ndarivoi alisema visima hivyo vinachimbwa katika eneo la Msikiti  na kituo cha afya Themi Mashariki, ambapo idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo wanachangamoto ya maji.

Ndarivoi alishukuru kwa msaada huo uliotolewa na mfadhili huyo, Nasr Al Jahadhamy na kueleza kuwa kilichomsukuma kuomba msaada huo ni upendo kutoka kwa wananchi wake baada ya wananchi hao kulalamika uwepo wa changamoto ya maji kwa muda mrefu.

“Huyu Sheikh amekuwa mkombozi kwenye kata yangu amewahi kutuchimbia visima vingine shule ya Themi sekondari na msingi na kilichonisukuma kutafuta mfadhili huyu tena ni upendo kwa wananchi wangu kwa sababu niliomba uongozi niweze kuwatumikia wananchi wangu”

Awali mfadhili wa visima hivyo,  Nasr Al Jahadhamy ,alisema alipokea maombi kupitia kwa Sheikh Ayubu Hussein juu ya uhitaji wa visima katika kata hiyo ndipo alipokubaliana na ombi hilo na kuamua kuja nchini kitekeleza ahadi hiyo niliyoombwa.

Alisema hadi sasa ni mwaka wa nane amekuwa akijishughulisha kusaidia kuchimba visima hapa nchini na kwa Mkoa  wa Arusha amechimba  visima vipatavyo 61 kwenye shule zaidi ya visima 10, Misikiti na maeneo ya wazi lengo ni kusaidia jamii yenye uhitaji.

“Mipango yetu ni kuendelea kusaidia kuchimba visima virefu na mwaka jana nilistaafu kazi Omani na nitakuwa na muda mzuri wa kusaidia “alisema.

Naye Sheikh Ayubu alisema kwa muda mrefu Jiji la Arusha limekuwa na changamoto ya maji hivyo waliona umuhimu wa kuwa na Mfadhili atakayewasaidia kuchimba visima vya maji kwenye misikitini na mashule ili watu wote wapate huduma hiyo.

“Kilichotusukuma ni shida ya maji kina mama kutoka usiku kutafuta maji ndio maana tuliamua kumtafuta ndugu yetu mfadhili kutoka Oman na kuja Arusha tulianza kuchimba vizima maeneo mbalimbali hadi leo ni kisima cha 61”

Mmoja ya mwananchi wa Themi Mashariki,Grace Rukwembe alisema kukamilika kwa kisima hicho kutawasidia kupunguza adha ya maji waliokuwa nayo.

Alisema awali waliyapata maji kutoka kwenye maboma ya watu kwa kununua kwa gharama kubwa ,hivyo wamemshukuru diwani wao kwa kufanikisha msaada huo.

Habari Zifananazo

Back to top button