KENYA; Nairobi; TANZANIA imeahidi kuendelea kushirikiana na Kenya katika kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati wa hotuba yake kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Kenya.
“Hivyo basi, leo ambapo Kenya inasheherekea miaka 60 ya Uhuru wake, napenda nitumie fursa hii kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana bega kwa bega na Serikali ya Kenya katika kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wetu wa kidugu na kihistoria kwa manufaa ya nchi zetu mbili na watu wake,” amesema Dk Mwinyi na kuongeza:
“Sio tu kwamba sisi ni majirani, bali pia wananchi wetu ni ndugu na utamaduni wao unafanana. Hii ndiyo sababu ni vigumu sana kumtofautisha Mmasai, Mdigo, Mjaluo ama Msegeju wa Kenya na Mmasai, Mdigo, Mjaluo au Msegeju wa Tanzania.
Wote wanazungumza lugha moja.
“Lakini, hata wale Wanyama wetu, ambao sisi kule Tanzania tunawaita nyumbu, na wenyewe kila mwaka wamejiwekea utaratibu wa kuhama kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.
Nimeambiwa huwa wanatoka upande Tanzania kuja Kenya kwa ajili ya kupata ujauzito, na kisha wanarudi upande wa Tanzania kujifungua.
“Hii yote inadhihirisha kuwa sisi ni ndugu na ni wamoja. Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba serikali zetu pia zinashirikiana vizuri na zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu kwenye masuala mbalimbali ya kimataifa, hususan kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola na bila kusahau Umoja wa Mataifa,” amesema.
Comments are closed.