Wananchi wahimizwa kupima afya zao

DAR ES SALAAM: Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), hospitali ya Dar Group, Dar es Salaam itaendesha zoezi la kupima watu wenye magonjwa ya moyo na magonjwa mengine kwa siku mbili kuanzia septemba mosi hadi mbili,2023 hospitalini hapo,na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi.

Hata hivyo hospitali hiyo imeeleza kuwa imeboresha huduma za dharura kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura kwa kuongeza vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa kutosha kuifanya huduma hiyo kuwa ya kiwango cha kimataifa.

Tayari imefunga mitambo na mashine mbalimbali yenye thamani ya sh milioni 760 zikiwemo za eco tatu, mashine za kupima moyo kwa wagonjwa waliozidiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema hayo akiwa katika hospitali ya Dar Group wakati akizungumzia uboreshwaji wa huduma za dharura uliokwenda pamoja na kutoa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na dharura.

Kuhusu kupima amesema tatizo la moyo limeongezeka sana nchini, na hiyo inatokana na mtindo wa maisha kwa watu kutofanya mazoezi mara kwa mara, kutokula chakula bora, pombe kuzidi kiasi na hata uvutaji wa sigara .

Kuhusu uboreshwaji amesema tangu serikali ilipotoa Hospitali ya Dara Group kwa JKCI, wameendelea kuimarisha huduma kwa kuongeza mitambo mingi haswa inayotumika katika kitengo cha dharura na mashine zote zitatumika kusaidia wagonjwa waliozidiwa watakaopelekwa hapo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upasuaji na Msimamizi wa kitengo cha magonjwa ya dharura na wagonjwa mahututi, Dk Anjela Muhozya amesema tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho wamekuwa wakiwaona wagonjwa kuanzia tisa hadi 20 kwa siku na huduma zimeboreshwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button