Wananchi wasisitizwa tahadhari mlipuko wa kipindupindu Bukoba

BUKOBA, Kagera: Watu wanne wamelazwa katika hospitali ya Wilaya Bukoba Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera  baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu.

Mkuu wa Wilaya Bukoba, Erasto Sima amesema hadi kufikia January 8, 2024 tayari wamepokea wagonjwa wanne ambao wameonesha  viashiria vya kipindupindu ambapo mgonjwa wa kwanza alibainika January 4 mwaka huu katika Mtaa wa Kafuti Kata yu Bakoba baada ya kuugua na viongozi kupewa taarifa.

Amesema kuwa timu ya wataalamu iliingia kazini na kuchunguza tatizo ambapo watu walianza kuumwa ugonjwa unaofanana na kufanya serikali kutenga eneo maalumu katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya uangalizi wa afya zao.

Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua hasa kutibu maji ya kunywa,kunawa mikono kwa maji safi na salama na kutokula vyakula na matunda visivyo salama.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kafuti Kata ya Bakoba, Respikius Mchunguzi akizungumza amesema serikali ya mtaa wameanza jitihada za kukabiliana na mlipuko huo huku akidai kuwa tatizo lilianzia kwa mwanamke mmoja aliyekuwa amejifungua aliyeumwa tumbo Januari 01, 2024 na kupoteza maisha baada ya hapo mtoto wake aliumwa na wananchi waliokuja msibani baadhi walianza kuumwa na ndipo Januari 4 serikali ikaanza uchunguzi.

Ameongeza kupitia serikali ya mtaa huo tayari wameanza ukaguzi kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa afya kuhakikisha wanatoa elimu kwa mama ntilie, jamii majumbani,watoto shuleni,ukaguzi wa vyoo safi na maeneo yanayoketisha watu ili kuweka sawa afya za wananchi.

“Kiukweli serikali iko kazini mwanzoni hatukujua kama ni tatizo lakini baada ya kugundua mtaa wetu watu wameanza kuugua ugonjwa unaofanana tukatoa taaarifa na haraka serikali ulifika na kuanza uchunguzi, amesema Mchunguzi.

Mwishoni mwa mwaka 2023 mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ulitokea katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera na watu wanne walipoteza maisha na wengine kulazwa katika hospitali na vituo vya afya.

 

Habari Zifananazo

Back to top button