‘Wananchi zingatieni utunzaji Mazingira’

ARUSHA: WANANCHI wametakiwa kuhakikisha wanazingatia na kutunza usafi wa mazingira ili kuepukana na athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza  kutokana na uharibifu katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha wanapanda miti

Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Usafi wa Mazingira iliyofanyika jijini Arusha,Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya kanda ya Arusha Joachim Tiganga aliyemuwakilisha Jaji mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,  alisema utunzaji wa mazingira unahusisha uoto wa asili  hivyo ni wajibu wa kila mwananchi  kuhakikisha anazingatia utunzaji wa mazingira kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza.

Alisema uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za binadamu kwa kiasi kikubwa ni katika kilimo, uchimbaji madini, ufugaji,pamoja na shughuli zingine za kila siku ikiwa ni pamoja na katika masoko kwa utupaji taka,pia ukataji miti nayo ni moja ya uharibifu wa mazingira.

“Uchomaji hovyo misitu ni changamoto nyingine kubwa katika uharibifu wa mazingira,pia utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa badala ya nishati mbadala ya gesi na umeme nayo ni chanzo cha uharibifu sambamba na uvunaji haramu wa miti usiofuata sheria nao chanzo kingine kikubwa katika kuharibu, “alisema Tiganga

Alisema katika takwimu zinaonyesha kuwa takribani tani milioni 7 za taka ngumu ndio ambazo huzalishwa nchini lakini pia kiasi hicho kinaonekana kwa kiasi kikubwa kuzalishwa kwenye majiji, manispaa, halimashauri za miji na halmashauri za miji midogo.

“Pia takwimu zinaonyesha ni asilimia 35 tu za kiasi hicho cha taka hukusanywa na kuteketezwa kwa utaratibu ambao ni salama,”alielezaTiganga

Alisema utunzaji wa mazingira unahusisha utunzaji wa uoto wa asili na kinachohitajika ni kuendelea kupanda miti.

“Naungana na mkuu wa wilaya ambaye ameelekeza kuwa kila kaya ipande angalau mti mmoja na kwa sababu haya ni maelekezo ya serikali  wananchi wayatekeleze, “alisisitiza Tiganga.

Habari Zifananazo

Back to top button