Wanandoa waliotelekeza watoto 5 wasakwa

OFISI ya ustawi wa jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imeanza kuwatafuta wanandoa wanaodaiwa kutelekeza watoto wao watano.

Wazazi na watoto wao walikuwa wanaishi katika Kitongoji cha Mwabuluki Kijiji cha Ng’wang’osha Kata ya Nyamalogo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Ofisa Ustawi wa Jamii katika halmashauri hiyo, Kulian Mlalama alisema hayo jana alipoitembelea familia hiyo akiwa amefuatana na Ofisa Mthamini na Mfuatiliaji kutoka Shirika la Thubutu Africa Intiative (TAI) la wilayani Shinyanga, Paschalia Mbugani.

Mlalama alisema wazazi hao wanatafutwa hata kama wameachana ili wawapeleke shule watoto hao na watimize wajibu wa kulea kwa ujumla.

“Sisi tutawaandikisha shule, tumeanza kuwatafuta wazazi tulikwenda kwa ndugu zao kwenye kijiji jirani kupata mawasiliano lengo ni watoto wapate haki zao za msingi ikiwemo elimu,” alisema.

Mtendaji wa kijiji hicho, Nyosoku Wambura alisema walifanya uchunguzi na wakabaini kuwa mama wa watoto hao ameolewa na mwanaume mwingine mkoani Geita na baba yao hajulikani alipo.

Mbugani alisema kitendo cha kutelekeza watoto na kusababisha wakose haki ya kupata elimu ni ukatili.

Mlezi wa watoto hao, Joyce Robert alisema anaishi na mumewe, Mashimba Usumahu anayefanya vibarua vya kulima na kwamba wao wana watoto sita hivyo familia imewaelemea.

Kwa mujibu wa Joyce, Mwenyekiti wa kitongoji, Marco Luhende ndiye aliyewapeleka watoto waliotelekezwa waishi kwenye familia yake.

Habari Zifananazo

Back to top button