Wanaofanya ‘uhausigeli’ Saudi Arabia hawatambuliki ubalozini

BALOZI wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Ali Jabir Mwadini, amesema hakuna utaratibu unaowatambua Watanzania waliokwenda kufanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia.

Balozi Mwadini alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanywa kwa njia ya video moja kwa moja kutoka Riyadh, Saudi Arabia.

“Nifafanue hili, fursa za ajira hapa Saudi Arabia zipo, na zilizofunguliwa  na serikali ya Tanzania kuridhia  na kuwataka wananchi wazichangamkie ni za udereva, uhudumu wa migahawa na hoteli. Sasa tumefungua kwa wauguzi na sekta ya afya, ila tunataka watu wapitie Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (Taesa),” alisema Balozi Mwadini.

Alisema hakuna Watanzania wanaofanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia waliokwenda kwa kutumia utaratibu rasmi wa kiserikali na kuwezesha ubalozi kuwa na taarifa zao bali wanaofanya  kazi hizo wamekwenda kinyemela.

“Kazi za ndani hatukufungua vibali kwa Watanzania kwenda kufanya na wala hatuna mikataba hiyo na hata kampuni zinazofanya uwakala wa wafanyakazi wanafahamu hilo kuwa hatukutoa vibali kwa kazi hiyo, ila tunasikia wapo ambao wanafanya kinyemela, sasa wakipata changamoto ndio ubalozi unaambiwa huyo ni Mtanzania,” alisema Balozi Mwadini.

Aliwasihi Watanzania kuepuka kudanganywa na kampuni au watu binafsi kuwatafutia kazi za ndani nchini humo na kuwasafirisha kinyemela kwa kujaza madhumuni mengine ya safari, kwani wakipata changamoto ni vigumu kuwatafuta walipo.

“Tutumie njia sahihi, fursa za ajira za wenye taaluma zipo ila fuateni utaratibu kuziomba na pia hakikisheni kampuni mnazoambiwa zinawatafutia kazi, zihakikini Taesa ili kuwa na uhakika na wakati mwingine kampuni hizo ndizo zinawadanganya kuhusu maslahi, wakifika na kukuta tofauti utata unaanza. Lakini wengine wanaondoka vizuri wakifika huko wanabadilisha mawazo na kutaka kufanya mambo mengine,” alisema Balozi Mwadini.

“Niwaambie kwa ujumla mazingira ya Saudi Arabia ni bora kuliko maeneo mengi. Kwa bahati mbaya masikio yanasikiliza habari mbaya. Hata mimi nilikuwa mzito kufungua soko la ajira kwa Watanzania. Wapo Watanzania 13, nilikutana nao baada ya kusikia changamoto zao na nilifuatilia na baadhi yao walirudi nyumbani kwa sababu walikuwa chini ya viwango vya kazi,” alisema Balozi Mwadini.

Alisema hadi sasa wapo zaidi ya Watanzania 1,200 wanaofanya kazi nchini humo ambao wanatambuliwa rasmi na idadi hiyo itaongezeka hivi karibuni baada ya kusainiwa kwa mkataba mwingine.

“Niwatake Watanzania wasikubali kutumia njia zisizo rasmi kuja kufanya kazi huko, kwa kutumia njia hizo wanaweza kukutana na changamoto, ila wakitumia mfumo rasmi, taarifa zao tunakuwa nazo na tunafuatilia na wanakuwa salama zaidi, ila kufanya kazi kinyemela sio jambo jema,” alisema Balozi Mwadini.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x