Wanaohamishwa wapewe taarifa mapema – Prof Tibaijuka

DAR ES SALAAM: ALIYEKUWA Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema serikali inapohitaji kuwahamisha raia kutoka eneo moja kwenda lingine inapaswa kuwapa taarifa mapema, lakini pia kuwalipa fidia stahiki ili wawe na nidhamu ya kukubali maagizo hayo.

Prof Tibaijuka amezungumza hayo katika kongamano la vijana kujadili fursa za kiuchumi, masuala ya uongozi na stadi za maisha, lililohusisha mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam.

“Kwa mfano unawahamisha watu kutoka Bonde la Msimbazi, huwezi kuwatoa bila taarifa huwezi kuwatoa bila fidia, lakini unapotangaza kwamba wanahama, ukatoa fidia stahiki, ukawatafutia makazi mbadala lazima pia raia wakuunge mkono wawe na nidhamu sasa,” amesema Prof Tibaijuka.

Advertisement

Sambamba na hilo Prof Tibaijuka amezungumzia suala la utunzaji mazingira ambapo amesema suala hilo linahitaji bajeti ya kutosha kutoka serikalini ili kuhimili katika kila eneo.

Pia amewataka vijana kuwa kipaumbele na kujenga utamaduni katika kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.

“Sasa kuna sehemu zingine tunashindwa kwa sababu bajeti zinakuwa hazitoshi, lakini sio suala la kama tu tutaweka utamaduni niliousema,” amesema Prof Tibajiuka.

Prof Tibaijuka amewataka vijana kujifunza lugha tofauti zaidi ili kufungua fursa maeneo mbalimbali katika kutafuta stadi za maisha ndani na nje ya nchi.