Wanaoharibu miundombinu ya maji kudhibitiwa Missenyi

Wanaoharibu miundombinu ya maji kudhibitiwa Missenyi
MKUU wa Wilaya ya Missenyi, William Sakulo amesema vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na kamati za watumia maji za vijiji, vitaanza kufanya masako na kuchukua hatua za kisheria wananchi wanaokata mabomba na kuharibu miundombinu mingine ya maji.
 
 
Mkuu huyo wa Wilaya akiambatana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya wilaya hiyo, alitembelea na kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Ruwasa katika vijiji vya Kitobo, Kashasha, Kijunja na Kyazi ambayo itahudumia kaya 973.
Amesema serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha miradi ya maji inakamilika, hivyo hataona aibu kumchukulia hatua mwananchi yeyote anayethubutu kuharibu miundombinu ya maji.
Ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Ruwasa na kusema kuwa linapokuja suala la upatikanaji wa maji na ubora wa miradi ya maji Missenyi vijijini ,anapata usingizi kwani watendaji wa Ruwasa wanafanya kazi usiku na mchana.
 
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Missenyi, Andrew Kilembe amesema kuwa miradi ya maji katika wilaya hiyo inaendelea kutekelezwa kwa kas,i ambapo asilimia 70 katika wilaya hiyo wanapata maji safi na salama ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita, ambapo hakukuwa na upatikanaji wa maji ya uhakika katika vijiji .
Amesema kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa Ruwasa kwenye vijiji 77 vinavyopaswa kupata huduma ya maji, tayari vijiji 42 vinapata huduma ya maji safi na salama na miradi mingine ipo katika utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024 .
 
Amevitaja baadhi ya vijiji vilivyopata maji kuwa Byamutemba, Igayaza, Mutukula, Kassambya, Bunazi, Omundongo, Nyabihanga, Kyaka, Kashaba, Bulifani, Kakunyu, Bugango, Kilimilile, Kenyana, Nyakere, Kibeo, Bulembo, Rukurungo, Igulugati, Mbale na Kijunja.
 
Vingine ni Kashasha, Kitobo, Kyazi, Rutunga, Rwamachu, Mugongo, Ruhija, Katolerwa, Luhano, Katano, Nyarugongo, Kabyaile, Kashekya, Kashaka, Kashambya, Kataale, Katendaguro Kigarama, Bweyunge, Bugombe na Kikukwe.
 
Katibu wa CCM Wilaya ya Missenyi, Bakari Mwacha amewataka viongozi kuwafuatilia wote wanaofanya uharibifu wa miondombinu kukamatwa mara moja, kwani uwepo wa maji safi na salama ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2020-2025
5 comments

Comments are closed.