Wanaoishi mipakani watakiwa kutumia fursa

CHAMA Cha mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma kimewataka wananchi wanaoishi maeneo ya mpakani, ambako kumejengwa masoko kwa ajili ya biashara ya ujirani mwema na nchi ya Burundi kutumia fursa ya uwepo wa masoko hayo kufanya biashara ambazo zina fursa kubwa ya kubadilisha maisha yao kiuchumi.

Katibu wa CCM Mkoa Kigoma, Mobutu Malima ametoa kauli hiyo alipofanya ziara kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kimkakati katika Kijiji cha Mnanira, Tarafa ya Manyovu Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Akizungumza baada ya kutembelea na kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, Malima alisema kuwa ujenzi wa soko hilo unayo nafasi kubwa ya kuongeza kipato cha wananchi wa maeneo hayo na wilaya ya Buhigwe kwa jumla, kwani kwa sasa Burundi ina fursa kubwa ya masoko kwa bidhaa za vyakula na za viwandani kutoka Tanzania.

Advertisement

Alisema kuwa tafiti zinaonesha kuwa wananchi wa mikoa ya Burundi inayopakana na Kigoma wamekuwa wakifanya manunuzi makubwa kwenye masoko mbalimbali ya mkoani Kigoma, hivyo kusogezwa karibu na mpaka kwa biashara hizo ni fursa kubwa kwa wananchi hao.

 

Alisema kuwa chama hicho kitaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya kuhakikisha serikali inaweka mazingira mazuri ya kufanyika kwa biashara za ndani na zile za kuvuka mpaka, ili kuimarisha shughuli za kiuchumi za Watanzania.

 

Akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Msanifu Majengo wa halmashauri ya wilaya Buhigwe, Kheri Kiliza alisema kuwa jumla ya shilingi Bilioni 2.3 zinatarajia kutumika kwa ajili ya ujenzi huo.

 

Kiliza alisema awali kiasi cha shilingi bilioni 1.7  kilitolewa na mradi ukasimama baada ya kutokea ubadhirifu na waliofanya hivyo walichukuliwa hatua na kwamba serikali imetoa milioni 600 kukamilisha ambapo utakamilika mwisho wa mwezi April.

 

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru alisema kuwa baada ya kukwama kwa miaka kadhaa mradi ulianza baada ya kuomba fedha na ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu lakini ameeleza kushangazwa na taarifa kwamba mradi huo utakamilika mwezi April.