Wanaopandisha bei ya sukari Moro kukiona

MOROGORO: MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameweka hadharani namba yake ya simu ya kiganjani kwa wananchi wa mkoa huo ili wampigie na kumtumia ujumbe mfupi wanapouziwa sukari kwa bei ya juu na wafanyabiashara tofauti na bei elekezi ya Sh 2,700 hadi 3, 200 ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Malima ametoa namba yake ya simu wakati maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi(CCM), iliyofanyika kimkoa mjini Morogoro na mgeni rasmi akiwa mlezi wa CCM mkoa huo na Mwenyekiti wa Taifa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Mohamed Ally Kawaida.

Amesema licha ya mkoa kuwa na viwanda vinne vya sukari ikiwemo cha Mtibwa, Kilombero I na II pamoja na kiwanda kipya cha Mkulazi lakini kuna changamoto ya upungufu wa sukari na kuifanya Serikali kuagiza tani 100,000 kutoka nje.

Malima amesema tayari awamu ya kwanza ya shehena ya sukari kutoka nje imeshawasili na serikali ilitoa bei elekezi ya kuuzwa kwa Sh 2,700 mpaka 3, 200 na kwamba bei hiyo ni sheria, hivyo wafanyabiashara wote wanapaswa kuuza kwa kuzingatia bei hizo.

“ Nasisitiza kuwa Serikali imetoa maelekezo mahususi kuwa sukari inauzwa mwisho Sh 3,200 kwa kilo na mwananchi wa Morogoro ukikuta inauzwa Sh 3,500 au sh 5,000 nipingieni simu mimi mwenyewe kwa namba yangu 0784 612020 kwa ajili ya kuniarifu sukari inauzwa kwa bei ya juu na nitaenda na kuwashukia mimi mwenyewe” amesema Malima.

Mkuu wa mkoa ameelezea upungufu uliojitokeza wa sukari nchini umechangiwa na viwanda kushindwa kuvuna miwa kutokana na mashamba yake kujaa maji kwa sababu ya mvua nyingi za mafuriko na kusababisha miwa hiyo kukwama kupelekwa viwandani kwenye uzalishaji sukari.

Malima amesema asilimia 70 ya sukari yote nchini inazalishwa katika mkoa wa Morogoro na kwamba miezi mitatu iliyopita hakuna uzalishaji kutoka na mashamba ya miwa ya viwanda hivyo na mashamba ya wakulima wa nje wa miwa yamejaa maji.

“ Mimi ndio Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro,nazunguka maeneo hayo kila siku na nimejionea Kiwanda cha Kilombero I na II,Mtibwa na Mkulazi mashamba yao yote yamezingirwa na maji na hakuna mashine wala Treka inayoingia mashambani “ amesema Malima.

Malima amesema kuanzia mwezi Novemba na Desemba (2023) , Januari na Februari mwaka huu zaidi ya tani 60,000 hadi 70,000 zilizopaswa kuzalishwa zimeshindikana kutokana na changamoto za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya mkoani Morogoro.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kawaida amewaomba wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Morogoro watoke maofisini kwenda kufanya msako kwa wafanyabiashara wanauza sukari kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya maelekezo ya serikali.

“ Tokeni ofisini msisubiri kupigiwa simu,nendeni mkafanye msako kukamata wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei isiyo elekezi ili tuweze kukomesha tatizo hilo” amesema Kawaida.

Habari Zifananazo

Back to top button