MKURUGENZI wa Kitengo cha Huduma za Ajira (TAESA), Joseph Nganga amewashauri vijana wa kitanzania wanaopata fursa za kazi nje ya nchi kuzingatia maadili ya kuchapa kazi na kufuata sheria za kazi, ili waweze kufungua fursa nyingi za kazi kwa vijana wengine.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, wakati wakiwasafirisha vijana 50 kati ya 408 waliosafirishwa kwenda nchini Saudi Arabia kufanya kazi katika Kampuni ya Kilimo Ufugaji na Usindikaji ALMARAI, Nganga amesema fursa hizo za ajira za nje ni adimu sana kuzipata, kwa hiyo amewataka vijana hao kuchapa kazi.
“ Ili mtu afanikiwe kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi, jambo la kwanza kabisa muhimu waajiriwa wote wanamtafuta mtu mwenye bidii, mtu anayejua kazi ueledi, ”alisema
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Bravo Job Centre, Abbas Mtemvu amesema tangu kuanza kupeleka vijana nje ya nchi kufanya kazi wengi wao wamekuwa wakifanya kazi kwa uadilifu
“Vijana waliochaguliwa ni 408 na tunatarajia vijana hawa wakimalizika tutakuwa na interview kubwa sana vijana 1800 wakiwemo madereva, salesman na labour, uzuri wa vijana hawa wanaokwenda kule wengine wana elimu na wasiokuwa na elimu kwa hiyo mimi nawaomba vijana hawa wajitokeze kwa wingi kuomba ajira hizi,” amesema.
Wakizungumzia kuhusu maandalizi ya safari yao , baadhi ya vijana hao wamewataka vijana wenzao kuthubutu kujitokeza kuchangamkia fursa za ajira za nje ambazo zina uhitaji mkubwa wa watu.
Pia wametoa pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kwa kufungua fursa hizo za ajira za nje, ambazo zitaweza kulisaidia taifa kukabiliana na upungufu wa ajira nchini.
Mpaka sasa vijana wapatao zaidi ya 200 wameshasafiri nje ya nchi kati ya vijana 408 ambao wamefanikiwa kupata kazi nje ya nchi kupitia Kampuni ya Bravo Job Centre chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Huduma za Ajira (TAESA