Wanaotaka kulipiwa mahari wafikia 1,000
IMEELEZWA kuwa hadi sasa watu zaidi ya 1,000 wameonesha nia ya kutaka kuoa kwa kulipiwa mahari na Taasisi ya Kiislamu ya Al-Hikma Foundation, baada ya wiki iliyopita taasisi hiyo kutangaza kulipia mahari vijana 50.
Akizungumza leo mwenyekiti wa taasisi hiyo, Shekhe Nurdin Kishki amesema watu hao walituma maombi kwa njia mbalimbali ikiwemo akaunti za mitandao ya kijamii ya taasisi hiyo, kupiga simu na kutuma jumbe mfupi za maandishi.
Kishki amesema masharti yapo manane, akataja baadhi kuwa sharti la kwanza, muoaji lazima awe muislamu, lakini pia asiwe na mke kwa maana mwanaume anayeongeza mke wa pili
Alisema amechagua muoaji kuwa muislamu kwa kuwa ndoa hiyo itafungishwa na mufti, hivyo haipaswi kwa asiyekuwa muislamu kufungishwa ndoa na muislamu.
Taasisi hiyo ilitangaza nia ya kuwalipia mahari vijana 50, Aprili 9, 2023 jijini Dar es Salaam katika mashindano ya 23 ya Afrika ya uhifadhi wa Qur’an kama sehemu ya programu yao ya kuleta manufaa kwa jamii kupitia mashindano hayo.