Wanasheria wataja vigezo, masharti kuandika wosia

WATANZANIA wamehimizwa kuandika wosia hata kama hawana mali ili kuepusha migogoro baada ya kifo.

Meneja wa Masoko na Elimu kwa Umma wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Wakili Josephat Kimaro alisema wosia unaweza kuwa wa namna mali zitakavyogawanywa mara baada ya mhusika kutangulia mbele za haki au unaweza kuwa utaratibu wa mazishi yake.

Kimaro alisema wosia wa utaratibu wa mazishi yatakavyokuwa unasaidia kuondoa sintofahamu zinazosababisha marehemu kuchukua muda mrefu bila kufanyiwa huduma hiyo kutokana na kuibuka kwa mivutano baina ya wanafamilia kuhusu mahali pa kuzikwa.

“Kinachokuwamo ndani ya wosia ni ama namna ya kugawa mali baada ya mhusika kuaga dunia au unaweza kuwa utaratibu fulani wa namna mambo yatakavyokuwa baada ya mhusika kufariki dunia,” aliongeza Kimaro.

Vigezo na masharti ya wosia

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe anasema ili wosia uweze kuhifadhiwa, lazima utimize vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na mashahidi kuanzia watatu kulingana na aina ya wosia, mfano wosia wa kidini, wosia wa kimila na wosia wa serikalini.

Anasema ili wosia upate hadhi ya kuwa wosia lazima usijulikane kwa mtu yeyote zaidi ya mwandika wosia pekee na kwamba hata mashahidi hawastahiki kujua, kusikia au hata kuona chochote kilichoandikwa ndani ya wosia.

Nani anastahiki kutunza wosia

Wakili wa Kujitegemea Constantine Kakula anasema wosia baada ya kuandikwa unaweza kutunzwa na mtu binafsi aliyeaminiwa na mwandika wosia, taasisi za fedha kama benki, wanasheria, taasisi za ibada kama makanisa na ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

“Kikubwa ni kuwe na mtu au watu wanaojua kuwa kuna wosia umehifadhiwa mahali fulani na mtu fulani ili ikitokea mtu huyo akafariki dunia kuwe na watu wa kufikisha taarifa kuwa marehemu aliacha wosia mahali fulani,” anaongeza Kakula.

Nani anaruhusiwa kuandika wosia?

Meneja wa Masoko na Elimu kwa Umma wa RITA, Kimaro anasema kila mtu ana haki na wajibu wa kuandika wosia na kwamba jukumu hilo si la watu wenye mali au matajiri kama baadhi ya watu wanavyofikiri.

Akawataka Watanzania kuandika wosia utakaoweka wazi mgawanyo wa hicho kidogo kilichopo kwa sababu baada ya kufariki dunia, baadhi ya ndugu na jamaa hawataangalia udogo wa mali zilizoachwa.

Wakili wa Kujitegemea Constantine Kakula anasema wosia unaweza kuandikwa na mhusika mwenyewe akiainisha namna mali zake zitakavyogawanywa na watu watakaohusika au kunufaika na mali zake lakini pia mtu anaweza kuandikiwa wosia na taasisi zinazotambulika kisheria kama ofisi za wanasheria na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Habari Zifananazo

Back to top button