Wanasheria watakiwa kutosheka na vipato vyao

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amewataka wanasheria wa Serikali kuwa waadilifu katika kazi zao ili wawe na nguvu ya utashi wa kuchukua hatua na kusisitiza kutosheka na kipato halali.

Dk Feleshi ameyasema hayo leo Septemba 29, 2022 mjini Dodoma katika mkutano wa wakurugenzi, mameneja na wakuu wa vitengo vya sheria serikalini na kusema uwadilifu katika kazi zao ni jambo muhimu ili kuwa na .nguvu ya utashi ya kuchukua hatua pale panapohitajika.

” Pia muwe na uadilifu ili kuwa na moral authority (nguvu ya utashi) na pia tumieni kipato chako halali kuendeleza familia yako, najua  fair life(maisha sawa) ni haki yetu lakini iwe kwa vipato halali.

Advertisement

” Mtu hawezi kuwa na utashi kama si mwadilifu, sasa wewe mla rushwa, halafu aunamwambia mtu fanya hivyo, si anasema wewe ni wale wale. Lakini kama umesimama lile neno lako la weledi litasimama.”

Aidha, Dk Feleshi pia ameonya wakurugenzi, mameneja na wakuu wa vitengo vya sheria serikalini  kuepuka kujenga uadui, mifarakano na uchochezi na kuwataka wanaoona kuna mambo yamewashinda kuondoka kuliko kuleta chokochoko kwenye ofisi ya umma.

“ Epuka kujenga uadui na mifarakano. Unajua kazi tuliyopewa ni ya Mungu. Mungu ni wa amani. Yaani kuna vitu ukiona wewe vinakushinda nafuu uache kazi uondoke lakini kuliko kuwa chanzo cha chokochoko kwenye ofisi ya umma.”

Alisema kwa kazi wanayoifanya mtu aamini kwa muonekano wa wakili atapata haki yaki na kwa neno lake mtu ajenge matumaini.

“Sasa wewe unakuwa ni mtu wa mafarakano, utakuwa unajenga ama unabomoa? Mengine ninayasema kwasababu hii kauli mbiu yetu mjue thamani yake kuna watu ambao hawataipenda.”

Dk Feleshi pia aliwataka mawakili wa serikalini kufurahia kukosolewa na kufanyia kazi maeneo ambayo wamekuwa wakikosolewa na watu na kama hawawezi wamuombe Mungu ili waweze kuyafanya hayo.

Alisema jambo hilo ni la afya kwa sababu kazi yao itakuwa ni ya kuyapima yale wanayokosolewa nayo na iwapo ni ya upuuzi basi wayapuuze.

Aidha, Dk Feleshi aliwataka mawakili  wa Serikali kujitathimini kama wanaendana na dhima na kujitosheleza kwa nafasi walizopewa.

“Jitathimini mwenyewe, kuna wagumu wa kujitathimini kwasababu ni mabwana wasio na makosa, basi waambie wengine wakutathimini. Huwezi wewe kujitathimini weka mifumo ya wewe kupata mrejesho.”

Alisema kwa kuweka mifumo ya kujitathimini kiongozi atajua udhaifu wake upo wapi na kuchukua hatua ili aweze kwenda mbele.

Dk Feleshi pia aliwataka viongozi hao kuweka mikakati ya kujengeana uwezo kwa warsha, kuwasimamia, semina na mikutano.

“Kuna watu wa ajabu kabisa Mungu amekujalia umesoma, halafu hutaki wenzako wapige hatua ni sawa na ibilisi kabisa. Kwasababu siku ya mwisho Mungu atakuhoji wangapi ulichangia wakaelewa kazi.”

Awali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Shaban Ramadhan Juma, alisema kikao hiko ni muhimu kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“ Mkutano huu ni muhimu Sisi tutajifunza wenzetu mnavyofanya kazi ili na sisi tuweze kuiga utendaji wenu mzuri.”

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini, Sylvester Mwakitalu na Naibu Wakili Mkuu, Dk Boniphace Luhende alisema kikao ni muhimu kwa kupanga mikakati ya namna utekelezaji mzuri wa masuala ya sheria.