Wanatuita maskini, lakini wanakuja kwetu!

MWISHONI mwa juma, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge la Tanzania.

Katika hotuba yake, alisema Tanzania inaungana na Serikali ya Uganda kuwa, mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani, Tanga (Tanzania) unatekelezwa kwa kuzingatia sheria zote za Tanzania na za kimataifa.

Aidha, unazingatia uwazi, tahadhari za kimazingira, ulinzi wa mifumo ya kiikolojia na rasilimali za maji, masuala ya kijamii, kijinsia na haki za binadamu.

Msimamo wa serikali umekuja siku chache baada ya Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) kupigia kura azimio la kusimamisha ujenzi wa EACOP kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na athari mbaya za kimazingira.

Majaliwa alisema mradi huo umefanyiwa tathmini ya kina ya kimazingira na kuhakikisha utekelezaji wake hauna athari za kimazingira.

Kwa Tanzania, mradi unagusa watu 9,513, zikiwemo taasisi mbalimbali, lakini kati yao, 331 sawa na asilimia 3.5 pekee ndio watakaohamishwa.

Alisema wanaoguswa na mradi huo walishirikishwa, kuchagua kujengewa makazi mapya au kupewa fedha taslimu na asilimia 85 walichagua kujengewa makazi.

Kwamba, nyumba 37 kati ya 309 zimekamilika na kukabidhiwa kwa wahusika na 55 zipo kwenye hatua ya umaliziaji huku 217 zikiwa katika hatua za awali za ujenzi.

Kimsingi, mradi huo ni muhimu kwa manufaa ya Uganda na Tanzania katika kukuza biashara, viwanda vya uzalishaji, kuongeza ajira na kuvutia wawekezaji wanaotarajiwa kukuza teknolojia na ujuzi kwa wananchi.

Ukweli huu ukiongezwa na wa upande wa Uganda dhidi ya uzushi huo, ndio unanifanya niseme kuwa, azimio la Bunge la EU linalenga si tu kwa EACOP, bali kustawisha ukoloni mamboleo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Afrika kwa ujumla.

Wazungu wanafanya hivyo, kwa kuwa hawataki kuona nchi za EAC na Afrika zikijikomboa kiuchumi badala yake, wanataka ziendelee ‘kukonda’ na kuwa tegemezi kwao.

Wanataka waonekana walinzi wa mazingira, lakini ndio wanaongoza kwa uchafuzi. Hawajui huwezi kuwa na mapinduzi ya kuondoa sultani, huku ukiendeleza usultani wa aina nyingine.

Wanachofurahia ni kuona umaskini na migogoro ya Afrika ili wajidai wanakuja kuilinda amani, kumbe wanakuja kuchota rasilimali na utajiri wa Afrika; tangu lini tajiri akawa mlinzi wa maskini? Wanataka kuja kwetu, lakini wanatuta maskini; mbona wanakuja kwetu.

Hao, wanajidai walinda amani, lakini nyuma ya pazia ndio wachonganishi ili Waafrika wapigane, wauze silaha na kuja kichota rasilimali.

Kimsingi, hawataki kuna EAC na Afrika zikicheka na kunenepa kiuchumi.

Nchi za EAC zikumbuke kuwa, mwenzio akinyolewa, wewe tia maji.

Hata hivyo najiuliza, mbona wanatuita maskini, lakini wanakuja kwetu?

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button