Wanawake 116 kupatiwa mafunzo ya uongozi
DAR ES SALAAM; JUMLA ya wanawake 116 watapatiwa mafunzo yanayolenga kuwawezesha kuingia katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na kuratibiwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), ikiwa ni program ya 10 tangu kuanza kwa mafunzo hayo.
Mtendaji Mkuu wa ATE,Susann Ndomba amesema leo Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa awamu hiyo pamoja na kuingia makubaliano na Bodi ya Wahandisi (ERB), yenye lengo la kutoa mafunzo hayo kwa wahandisi wanawake.
Amesema makubaliano hayo ni ya miaka mitatu kuanzia 2024-2026 ,ambapo kila mwaka ERB watakuwa wanaleta wanawake 13 katika programu hiyo yenye lengo la kuwajengea kiuongozi wanawake.
Amesema katika makubaliano hayo wahandisi wamewekeza dola za marekani 39,000, ili kutoa mafunzo kwa wanawake 13 na ATE inatoa nafasi moja kila mwaka ya upendeleo kwa wahandisi.
Amesema program imeweza kuwavutia walio wengi na kampuni zinawekeza kwa wanawake, hivyo inawafundisha wanawake katika maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi na mawasiliano.
“Lengo ni kuhakikisha kwamba tunaweza kutoa na kuongeza ujuzi kwa wanawake katika masuala ya uongozi, wataingia darasani kwa miezi tisa, viongozi mbalimbali watazungumza nao,”amesema na kuongeza kuwa kuwekeza kwa wanawake , inaongeza tija katika sehemu za kazi.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB ) Bernard Kavishe amesema wanaingia katika programu hiyo Ili kuchagiza wanawake kulindwa na mazingira mbalimbali ya uongozi.
Amesema kutokana na hilo ndio maana kwa uwezo walionao ATE, makubaliano hayo yamefikiwa, ili kuwapika kwa kuwa wanawake wanaweza na wajivunie uwepo wa viongozi wa nchi wanawake kuendelea kujiimarisha.
Amewataka Watanzania kutumia vyema bahati ya kuwa na viongozi wanawake akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge,Tulia Ackson, ambao wamekuwa chachu ya kuonesha uwezo wa wanawake na fursa hiyo itumike vizuri, ili kuleta usawa wa kijinsi na kuongeza dalili za maendeleo.
.”Ili kufikia usawa wahandisi wamekuwa na miradi ya kutatua tatizo la usawa kwa wanawake na wanaume katika sekta hiyo, ambapo kupitia makubaliano hayo kwa miaka mitatu taasisi itatoa wanawake hao ili kupewa mafunzo hayo,” amesema.