“Wanawake milioni 200 wamepitia ukeketaji na unyanyasaji”
DAR ES SALAAM: TAKWIMU za Kimataifa zinaonesha kuwa zaidi ya wanawake na watoto wa kike milioni 200 ulimwenguni wamekeketwa pamoja na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji.
Kati yao milioni 20 wamefanyiwa vitendo hivyo na wataalamu wa afya, ilhali zaidi ya wanawake na watoto wa kike milioni 60 wapo katika hatari ya kukeketwa.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 09, 2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima katika Mkutano wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji.
Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano huo, unaoratibiwa chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi 21 wameshiriki Mkutano huo wakiwemo Mawaziri nane barani Afrika.
Dk. Gwajima amesema ili kudhibiti na kutokomeza vitendo vya ukeketaji na unyanyasaji kwa wanawake na watoto wakike barani Afrika, nguvu lazima iongezwe katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo viovu.
Kiongozi huyo amesema hayo yatafikiwa kwa kuwa na mfuko imara utakaowezesha kuifikia jamii na kuielimisha kwa kutumia mfumo shirikishi ikiwemo kushirikisho wanaume katika mapambano haya.