Wanawake wahamasishwa ufugaji wa nyuki

‘Sumu ya nyuki inatibu maumivu ya kichwa, misuli, magonjwa ya ngozi’

ALICE Kibipi mfugaji nyuki wilayani Butiama, mkoa wa Mara amewashauri wanawake wenzake kujikita katika biashara hiyo na kuachana na dhana kwamba hiyo ni  ya wanaume tu.

Ametoa wito huo leo Agost 26, alipotembelewa na maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini  (TFS) kujua maendeleo ya ufugaji wake,  pamoja na kumpatia elimu ya ufugaji kwa njia ya ‘nyumba ya nyuki’.

Kipibi ambaye ni mtumishi wa umma wilayani humo, amewasistiza wanawake wenzake kuingia katika shughuli hiyo, ambayo muda wake hauingiliani na saa za kazi, kwa waajiriwa.

Advertisement

“Shughuli nyingi za nyuki zinafanyika kuanzia jioni kwa ushauri wa wataalam na kuna faida kubwa kwa anayefuata kanuni za ufugaji bora, elimu ambayo mimi naipata kutoka kwa wataalam wa wakala,” amesema.

Amesema alianza na mizinga mitatu mwaka 2017 kama majaribio. Sasa ana mizinga 27 na kila mzinga unampatia lita tisa za asali kwa msimu.

Mazao mengine anayopata kwa wingi ni nta, mavuno yanayompa wazo la kuanzisha utengenezaji wa mishumaa na vipodozi vya mdomoni kwa wanawake (Lipstick).

Mhifadhi wa TFS Wilaya ya Butiama, Hafidhi Said, amefafanua kwamba ‘nyumba ya nyuki’, ni njia ya kuweka mizinga kwenye jengo moja, ili kurahisisha huduma kwa nyuki.

Baadhi ya huduma ni urahisi wa kukagua mizinga, ili kuhakikisha hakuna wadudu, hasa sisimizi na siafu, wanaoweza kuingia ndani na kuwasumbua nyuki.

“Kwa asili, nyuki hawataki usumbufu wa aina yoyote. Vinginevyo watahama mzinga haraka iwezekanavyo,” amesema.