Wanawake wajasiriamali watangaziwa neema

Wanawake wajasiriamali watangaziwa neema

WAJASIRIAMALI wanawake wametakiwa kutumia kikamilifu kituo cha kimataifa cha biashara kilichozinduliwa Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi kitakachowezesha kutangaza biashara zao katika soko la kimataifa.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Habiba Omar wakati aliposhiriki katika uzinduzi wa kituo hicho cha kwanza chenye lengo la kutangaza biashara za wawekezaji ikiwemo wanawake.

Alisema serikali ya Zanzibar imefungua milango ya uwekezaji na kuwa fursa hizo ni muhimu katika kujikwamua kiuchumi na uwekezaji. Alisema imetenga Sh bilioni 46 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali kuingia katika soko la biashara.

Advertisement

Aliongeza kuwa kuwepo kwa kituo hicho ni fursa nyingine muhimu itakayowawezesha wanawake kupiga hatua kubwa ya kibiashara katika kazi zao.

“Serikali ya Zanzibar imefurahishwa na kuwepo kwa kituo hichi ambapo tunaamini kitasaidia kuleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo za kibiashara kwa wajasiriamali kuonesha bidhaa zao na kuingia katika soko la kimataifa,” alisema.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar, Rahma Salim Mahfoudh alisema amefurahishwa na kuanzishwa kwa kituo hicho na taasisi ya uwekezaji katika eneo la maeneo huru ya Fumba ambayo ni sehemu ya mabadiliko makubwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

Alisema katika mikakati na mpango mkuu wa serikali ya Zanzibar inayotokana na dira ya maendeleo 2020-2030 pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 ni kuona kwamba wanawake wanawezeshwa na kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi.

Rahma alisema maeneo huru ya kiuchumi yaliyopo Fumba ni pamoja na kituo cha biashara cha kimataifa ambacho ni fursa nyingine muhimu ya kuleta mabadiliko makubwa ya kibiashara kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanawake.

Mwakilishi wa Jimbo la Dimani lililopo katika eneo la uwekezaji Fumba Mwanaasha, Khamis Juma alisema kituo cha biashara ni fursa nyingine za kwenda kuwakomboa wanawake kiuchumi na uwekezaji na kuingia katika soko la biashara kwa mafanikio makubwa.