WAJASIRIAMALI wanawake, vijana na wamachinga wameandaliwa namna bora ya kupatiwa elimu ya mikopo itakayowawezesha kuboresha mitaji yao na jinsi ya kulipa kwa urahisi ili kuepuka changamoto za ulipaji.
Hayo yamesemwa leo Januari 30, 2023 na Mkurugenzi wa Maendeleo Bank, Ibrahimu Mwangalaba wakati akiwasilisha kwa waandishi wa habari taarifa ya maendeleo ya benki hiyo kwa mwaka uliopita.
Mwangalaba amesema kuwa mpango wa kuwapa mikopo wamachinga ulianza mwaka uliopita. ambapo kiasi cha Sh bilioni 3 zilitumika kwa wamachinga 2500, hivyo kutokana na mafanikio mwakubwa ya mwaka 2022 wameamua kuongeza makundi ya wanufaika.
“Pamoja na hayo benki inakusudia kutoa bidhaa kwa ajili ya wamama na vijana, na kuwafundisha namna ya kuendesha mikopo hiyo na watapata kutokana vigezo ambavyo tutavizingatia,” amesema Mwangalaba.
Amesema lengo la benki hiyo ni kuwafikia wamachinga 5000 na kufafanua kuwa zaidi ya wanawake 3000 tayari wamefikiwa, na wamepanga kuwapa elimu wanawake zaidi ya 15,000 ambao watanufaika na mikopo.
Akifafanua mikakati ya mwaka 2023, Mwangalaba alisema wamepanga kuongeza matawi kwenye baadhi ya maeneo kabla ya Aprili mwaka huu, pamoja na kuanzisha huduma za mitandao ‘Sim Banking’ na namna nzuri ya ulipaji ada kwa wanafunzi.
Amesema taasisi yao imepata faida kutoka Shilingi milioni 580 hadi Shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka 2022 na kwamba mafanikio hayo yamekuja baada ya kutengeneza njia sahihi za uzalishaji.