“Wanawake wanauogopa uongozi”

DAR ES SALAAM: Licha ya kuongezeka  kwa idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi bado wanawake wameshidwa kutojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi .

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, wakati akisoma tamko  kwa niaba ya Mtandao wa Bajeti yenye Mtizamo wa Kijinsia, katika kuelekea siku ya wanawake Duniani.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa ‘Wekeza kwa Wanawake, Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”

Advertisement

Liundi amesema ni umuhimu kuwekeza kwa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa ili kuleta maendeleo shirikishi.

Hata hivyo, Liundi amesema upande wa wabunge wa kuchaguliwa, idadi ya wanawake ni 24 kati ya wabunge 264 ambayo ni sawa na asilimia 9.1 huku idadi ya wabunge wanawake wa viti maalumu ni 113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya wabunge wote na  jumla ya wabunge wanawake ni 141 sawa na asilimia 37 ya wabunge wote ambao ni 393.

“Kutokujitokeza kwa wanawake kuwania nafasi mbalimbali ya uongozi katika changuzi mbalimbali kunapelekea kuwepo Kwa idadi ndogo ikilinganishwa na lengo la kufikia asilimia 50/50″amesema

Akizungumzia upande madiwani  amesema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya madiwani wanawake wa kuchaguliwa kutoka kwenye kata ni 204 ambayo ni sawa ana asilimia 3.8 ya madiwani wote huku madiwani wanawake wa viti maalumu ni 1,407 sawa na asilimia 26.2 ya madiwani wote.

Aidha ametaja changamoto inayochangia kurudisha nyuma harakati za ukombozi wa wanawake ikiwemo umiliki mdogo wa wanawake kwenye Ardhi.

Pia amesema kwa wanawake kukosa umiliki wa ardhi kumekuwa kukisababisha  kukosa fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kwa ajili ya kujikwamua.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya TGNP, Gemma Akilimali amesema mojawapo ya jitihada muhimu zinazopaswa kufanywa ni kuchechemua mabadiliko ya sheria na sera hususani mabadiliko ya kikatiba yatakayo  weka mazingira wezeshi ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi ya maamuzi.