DAR ES SALAAM: Wanawake wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi barani Afrika wametajwa kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya uvuvi, hususan katika uchakataji na kilimo cha mwani.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Ofisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Jovice Mkuchu, akifungua kikao cha mtandao wa wanawake barani Afrika wanaochakata mazao ya uvuvi, kikiwa na lengo la kukuza uelewa kuhusu uongozi katika mitandao wanayoiwakilisha nchi zao.
Akimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Mkuchu amesema, serikali inatambua umuhimu wa wanawake katika kuwezesha na kuendeleza sekta ya uvuvi barani Afrika, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwezesha na kuinua wanawake kwenye kilimo cha mwani na shughuli za uvuvi.
Amesema Tanzania imefurahi kuwezesha kikao hicho cha siku tatu kinachodhihirisha namna inavyoshirikiana na nchi mbalimbali barani Afrika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET) wenye makao makuu nchini Tanzania, Editrudith Lukanga, amesema mtandao huo una wanawake 44.