Wanawake wasimamia kidete mradi wa maji 

TANGA: Wanawake wa Kata ya Kideleko halmashauri ya mji wa Handeni wamepanda  miti na kufanya usafi katika bwawa la maji la Kwamaizi  ikiwa ni kuazimisha Siku ya Wanawake Duniani
leo Machi 8,2024.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Handeni Yohana Mgaza amesema  bwawa la Kwamaizi ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Kideleko hasa wakinamama ambao wao ndio wana jukumu la kutafuta maji kila siku.
Amesema, kutokana na hali hiyo wameamua  kutumia siku hii kulishafisha na kupanda miti rafiki kuzunguka bwawa hilo ili liweze kudumu katika muda uliokusudiwa.

Bwawa la Kwamaizi katika halmashauri ya Handeni lilikamilishwa chini ya Ufadhili wa Kampuni ya bia ya Serengeti na kusimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la WaterAid ambapo tangu kukamilika kwake mwaka jana linahudumia takribani wananchi 1944.

Akizungumzia nafasi ya kinamama katika usimamizi wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Neema Kimaro amesema licha ya mradi huo kulenga huduma ya maji safi kwa wananchi, pia, kuliundwa kikundi maalum cha wakina mama 24 waliosajiliwa kwa kazi maalum ya kuwezesha jitihada za kusimamia maswala yote ya uhifadhi wa Mazingira na ulinzi wa miundombinu ya maji ikiwemo usafi katika bwawa.
“Kikundi hiki kitafanya majukumu yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira – HTM wakiratibiwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Mji wa Handeni, ” amesema Neema.
Nae Mwenyekiti wa usimamizi wa mradi huo ambae pia ni wanufaika
Fransisca Mhando amesema lengo la  kikundi chao ni kusimamia mauzo ya maji katika bwawa hilo  pia kusimamia matunzo na usafi wa mazingira kwa ujumla katika eneo linalozunguka bwawa.
Nchini Tanzania kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ni “Wekeza katika wanawake: Kuharakisha maendeleo”.
Advertisement