Wanawake watakiwa kujiandaa kupiga kura Mtwara

WANAWAKE  waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea mkoani Mtwara wametakiwa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura  ili waweze kupiga kura mwaka 2025.

Rai hiyo imetolewa leo Machi 8, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake  Duniani ambapo kimkoa yamefanyika katika kijiji cha Chigugu wilayani Masasi mkoani humo.

Advertisement

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Daisy Ibrahim ambaye ni Mwenyekiti wa UWT mkoani humo, amesema itapofika muda wa uandikishaji wa daftari hilo wanawake hao washiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

“Wanawake ambao hawakujiandikisha  kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2020 wafanye hivyo pale muda utakapofika wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura,”amesema.

Mmoja wa wanawake katika kilele hicho akiwemo Siri Shabani amesema wataendelea kuwashauri wanawake  wenzao ili wale ambao hawajajiandikisha katika daftari hilo wajiandikishe ili waweze kugombea nafasi hizo.

Kwa kufanya hivyo itasaidia  kupaza sauti ya kuwasemea watoto wao katika jamii wakiwemo wa kike na wakiume.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amewataka wanawake mkoani humo kupiga kelele kwa kufanya kazi kwa bidii zinazoonekana ili kuliletea taifa maendeleo.

Amesema pamoja na kufanya kazi lakini pia kuchangamkia fursa za mikopo ambayo kwa sasa inafanyiwa maboresho ili ianze kutolewa kwa wananchi.