Wanawake watakiwa kutumia fursa sekta zingine

WANAWAKE wametakiwa kukamata fursa katika maeneo mengine ya sekta ya uziduaji, ikiwemo gesi na mafuta, badala ya kujikita katika uchimbaji madini tu ambao mapato yake hayatabiriki.

Ushauri huo umetolewa na washiriki wa  mdahalo wa kujadili ushiriki wa wanawake katika sekta ya uziduaji, ulioandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la HakiRasilimali mkoani hapa, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Mshiriki kutoka Shirika la Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), Fatuma Mssumi, amesema mojawapo ya maeneo yenye fursa ambazo wanawake bado hawajazichangamkia ni wa mradi wa bomba la mafuta Hoima-Chongoleani (Uganda-Tanzania).

“Unatarajiwa kuwa na kambi takribani 12, ikiwemo ya wilayani Nzega, takribani kilometa ishirini tu kutoka mkoani hapa na itakua na watu si chini ya 1,000 wenye mahitaji tofauti,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), Kitengo cha Jiografia na Uchumi, Prof. Abel Kinyondo, yeye amewashauri wanawake kutojiwekea mipaka ya kijiografia katika  dhana nzima ya ushirikishwaji  jamii (local content), katika maeneo yenye migodi, hatua itakayokuza ushiriki wao kwenye kuongeza mnyonyoro wa thamani katika sekta hiyo.

Amesema wengi wamekua wakitafsiri dhana hiyo kwamba jamii inayopaswa kushirikishwa ni ile tu iliyozunguka migodi, hivyo  kushindwa kuwashirikisha watanzani wengine ambao huenda wakatatua changamoto zinazowakumba.

“Sheria inasema ushirikishwaji wa jamii ni kwa mzawa yeyote kutoka kona yoyote ya Tanzania. Wanawake msibaki nyuma, wasilianeni na walio nje ya mipaka yenu  wawatatulie  changamoto hasa ya ukosefu wa mitaji ili kukuza uwekezaji wenu migodini,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button