‘Wanawake wawe sehemu umiliki ardhi ya familia’
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeshauri katika utaratibu wa kurasimisha ardhi, wanawake wahusishwe kwenye kumiliki ardhi ya familia.
Akizungumza wakati wa kuzindua masijala ya kijiji ya kuhifadhia hatimiliki na kutoa hati kwa watu waliorasimishwa ardhi katika Kijiji cha Manyemba wilayani Chamwino, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Chaurembo alisema ni vyema kubadili mitazamo na kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya umiliki wa ardhi ya familia.
Masjala na hati hizo zimetolewa kutokana na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita).
“Mnapoandaa hizi hati, kama eneo ni la kifamilia na akina mama nao wamiliki kwa kuhakikisha majina ya watu wote wawili yanakuwapo kwenye hati, jina la mama linakuwapo na jina la baba linakuwapo,” alisema Chaurembo.
Aliongeza “Si dhambi kwa hati moja kuwa na majina zaidi ya moja, ndugu zangu tujenge utamaduni sasa wa kina mama wawe sehemu ya kumiliki ardhi zetu na hii ina maana kubwa kwa sababu akina mama ndio walezi wa familia.”
Chaurembo alisema kutolewa kwa hati hizo kunafanya maeneo yao kuongezeka thamani. Aliwataka wananchi kuzitumia kujiinua kiuchumi kwa kukopa kwenye taasisi za fedha.
Aliitaka Halmashauri ya Chamwino kuhakikisha inapanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi akisisitiza kuwa kufanya hivyo kutachangia maendeleo kwa wananchi.
Pia amewataka kutumia fedha zinazotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambazo hazina riba, kufanya uendelezaji wa miji kwa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi wananchi.
Alisema kamati yake inakwenda kuishauri serikali ili kijiji cha Manyemba kipandishwe hadhi na kuwa kata.
“Mbunge wenu (Deogratius Ndejembi) kila wakati ameiambia kamati kuwa wana Manyemba wanataka wapewe kata na sisi kama kamati tumeliona hilo baada ya kujionea hali halisi kwa kweli tutakuwa mabalozi kuomba kata hii igawanywe.”
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye ni Mbunge wa Chamwino, Deogratius alisema kazi iliyofanywa na Mkurabita imesaidia kuondoa migogoro ya ardhi iliyokuwapo katika wilaya hiyo.
Awali, Mratibu wa Mkurabita , Dk Seraphia Mgembe alisema katika kutekeleza mpango huo kwenye halmashauri, walizingatia utayari wa halmashauri, uwapo wa wataalamu, vifaa, uhitaji wa utatuzi wa migogoro, uwapo wa eneo kwa ajili ya masjala au vituo jumuishi na aina ya shughuli za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Urasimishaji Ardhi na Biashara wa Mkurabita, Jane Lyimo alisema wilaya ya Chamwino imerasimisha ardhi katika vijiji vya Membe, Mahama na Manyembe ambako mashamba 2,324 yamepimwa na hati miliki za kimila 1,656 zimetolewa kwa wananchi.
Alisema pia wakulima 294 na viongozi wa ushirika na vikundi vya wakulima 62 wamepatiwa wafunzo ya matumizi ya hati miliki za kimila kiuchumi.