Wanne kunyongwa kwa kumuua diwani

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu watu wanne kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Diwani wa Kata ya Usunga, Alfred Masamalo (CCM) wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Joviti Kato aliyekasimiwa mamlaka ya Jaji alisema kwamba adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wa aina hiyo kwa vitendo vya mauaji wilayani Sikonge kwani vitendo hivyo vimekuwa vingi.

Hakimu huyo aliwataja washitakiwa waliopatikana na hatia ni Abdallah Mussa (32), Ezekia Kavenga (40), Ramadhani Saidi (29) na Abdallah Habibu (30) wote wakiwa ni wakazi wa Kata ya Usunga katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Alisema kifungu cha sheria kilichowatia hatiani ni cha 1996 na 1997 cha sheria ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 – 2022.

Hata hivyo, Hakimu Kato alisema kwamba washitakiwa hao walikuwa wakienda nyumbani kwa diwani huyo mara kwa mara huku wakijipanga kwenda kufanya tukio ambapo wote walikuwa na mipango hiyo.

Alisema mshitakiwa namba moja alikuwa na tamaa ya kumiliki mifugo aliyokuwa akiangalia ambayo ni mali ya Masamalo.

Kato alisema washitakiwa hao walikuwa wakimvizia Masamalo katika maeneo mbalimbali ambayo walijua watafanikiwa azma yao waliyoipanga kuifanya ya kumuua ili wanufaike na mifugo na madaraka ya nguvu.

Washitakiwa wote walikwenda kukaa darajani wakimsubiri Masamalo na kufanikiwa kumpata wakati anarudi nyumbani kwake na walimkatakata mapanga hadi kufa.

Awali mawakili wa upande wa Jamhuri ukiongozwa na Alice Thomas na Steve Mzava aliiambia mahakama hiyo kwamba tukio hilo lilitokea Machi 6, 2020 wakati muda wa uchaguzi ulikuwa umefika.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Amos Gehese akiwa na Agnes Simba waliiomba mahakama itende haki kutokana na kosa lao ili iweze kuwa fundisho kwa watu wengine wenye dhamira kama hiyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button