Wanne mbaroni mauaji ya mwalimu kwenye magugu

JESHI la Polisi mkoani Mara limewakamata watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Ligangabilili, Itilima mkoani Simiyu, Monica Patrick yaliyofanyika mjini Musoma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Longinus Tibishubwamu alilieleza HabariLEO kwa simu jana kuwa asingetoa utambulisho wa watuhumiwa watatu kwa sababu za kipelelezi.

Mtuhumiwa mkuu, Mohammed John amejitambulisha kupitia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Advertisement

Kwenye video hiyo, Mohammed anakaririwa akikiri kumuua Monica na kuuzika mwili wake kwenye magugu maji kwenye Ziwa Victoria, eneo la Makoko mjini Musoma.

Shemeji wa marehemu, Osca Abinery, naye akizungumza na HabariLEO kwa simu jana asubuhi, alisema baada ya sampuli kwa ajili ya uchunguzi kuchukuliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara juzi jioni, walichukua mwili wa ndugu yao na kusafiri usiku kwenda kwao Kilimanjaro.

“Tunaingia nyumbani sasa hivi (jana saa 5 asubuhi), tutazika muda huu maana mwili haupo vizuri,” alisema Abinery.

Kuhusu watuhumiwa kufikishwa mahakamani, ASP Tibishubwamu alisema upelelezi bado unaendelea, licha ya waliokamatwa imebainika mauaji hayo hayakuanzia kwa Mwalimu Monica na wahalifu hao wana mtandao mkubwa hata nje ya Mara.

“Wanalenga zaidi wanaofanya shughuli za madini kwa hiyo wamekuwa wakipata hela nyingi… labda wiki moja kuanzia sasa tunaweza kukamilisha upelelezi uzuri watuhumiwa wanafunguka (wanajieleza),” alisema.

Alisema Mwalimu Monica aliuawa kando ya ziwa hilo baada ya kukutana na Mohammed kwenye basi, mkoani Shinyanga na kukubaliana afike Musoma kusomewa dua ili nyota yake ing’ae apate mafanikio kwenye biashara ya ununuzi wa madini.

Alisema walimtaka awalipe Sh milioni 10 lakini akalipa Sh milioni 9.5 na alipofika Musoma, Mohammed alimpokea na kuongozana naye mpaka Makoko alikopewa kinywaji kilichochanganywa na kiasi kikubwa cha dawa ya usingizi aina ya Valium, ikamlevya na kusinzia fofofo.

Kwa mujibu wa Mohammed (kwenye video), Monica alizikwa ndani ya magugu maji akiwa ameshakufa, hakuvuliwa nguo na alipohojiwa kuhusu nguo zilizokutwa eneo yalipofanyika mauaji alisema hazifahamu.

Familia ya Mwalimu Monica ilipongezwa na Kamanda Tibishubwamu kwa jitihada za kumtafuta na kwamba walishirikiana na polisi kufuatilia nyendo za mwisho wa uhai wake mpaka wakamfikia Mohammed ambaye alikiri na kuwaongoza mpaka walikomzika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa huo, ambako mwili ulihifadhiwa baada ya kuopolewa, Osmund Mganga, alilieleza HabariLEO jana kwa simu kuwa matokeo ya uchunguzi wa mwili huo uliofanywa hospitalini hapo juzi, yanatarajiwa kutumiwa kwenye ushahidi mahakamani.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *