Wanne wanaswa Iringa wakielekea Afrika Kusini
SAFARI ya raia wanne wa Ethiopia waliopenya nchini kwa lengo la kuelekea Afrika Kusini bila kuwa na vibali imeishia mkoani Iringa baada ya jeshi la Polisi kuwanasa katika kizuizi cha Polisi Changarawe wilayani Mufindi.
Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi alisema waethiopia hao walikamatwa Mei 22, mwaka huu wakiwa kwenye gari mbili tofauti (IT) zilizokuwa zinapelekwa Zambia.
“Waethiopia hao walikuwa wakielekea Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma kwa kutumia gari hizo ambazo ni IT 3802 aina ya Vits na IT 7485 aina ya mazda,” alisema.
Alisema wakati Vits ilikuwa ikiendeshwa na Musa Omari (32) mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Mazda ilikuwa ikiendeshwa na Musa Mashala mkazi wa Airport Dar es Salaam.
Wakati majina ya waethiopia wawili hayajajulikana kwasababu ya changamoto ya lugha, Kamanda Bukumbi aliwataja wawili wengine kuwa ni Tesfahun Petros (22) na Degefe Sugumo (20).
“Watuhumiwa hao kwa pamoja wanashikiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani pamoja na magari hayo yatapelekwa kama vielelezo,” alisema.
Wakati huo huo Kamanda Bukumbi alisema katika oparesheni ya jeshi hilo iliyofanywa kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha kati ya Mei 17 na 23 mwaka huu wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa ujangili wawili Nazareth Miliuka (64) na Jafari Miluka (24).
Alisema watuhumiwa hao wote wakazi wa kijiji cha Wangamaganga wilayani Mufindi walikamatwa wakiwa na silaha tatu aina ya gobole, unga wa baruti, goroli nne, mafundo mawili ya pamba, vyuma vidogo nane na mtego wa wanyama.
Vile vile katika msako uliofanyika katika kijiji cha Mapogoro kata ya Idodi wilayani Iringa walifanikiwa kumkamata Tony Vitus (48) mkazi wa Mbinga Ruvuma akiwa na meno makubwa manne na vipande saba vya Tembo.
Alisema uchunguzi wa matukio hayo unaendelea na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa pindi uchunguzi utakapokamilika.