Wanufaika Tasaf waomba fedha kuboresha mitaji

WANUFAIKA wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF) mkoani Mtwara wameomba kuongezewa kiasi cha fedha wanachopokea ili kuboresha mitaji yao.

Martha Leonard mkazi wa Mtaa wa Ofisi Kuu Kata ya Chikongola Manispaa ya Mtwara Mikindani amesema fedha hizo za msaada alinunua mkokoteni ambao unamsaidia kurahisisha kazi yake ya ukusanyaji wa takataka kwenye maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

‘’Tunaishauri TASAF iweze kutuongezea hela ili niweze kununua vifaa ambavyo vitarahisisha kazi yangu hii ya kusomba takataka kwa mkokoteni’’ amesema Martha

Sauda Ally mkazi wa kata hiyo ambaye pia ni mfanyabiashara ya mahindi amesema anaendeleza biashara yake kupitia fedha hizo za msaada lakini kikubwa amesisitiza suala la kuongezea fedha ili wazidi kuboresha mitaji yao ili kuwaendeleza kimasomo vijana wao.

Mwanahamisi Abdallah mkazi wa Kata ya Magomeni katika manispaa hiyo ambaye alianza kunufaika mwaka 2014 kwa kuwezeshwa Shilingi 20,000 isiyo na masharti, kisha 36000, lakini hadi leo anapata Shilingi 10,000 tu ya Mwanafunzi wa Shule ya Msingi.

“Nawashukuru TASAF wawe na moyo huo wa kuendelea kutusaidia, tunashindwa kufanya miradi mikubwa kwa kuzingatia pesa ambayo tunapewa mimi nasomesha, nauguza, nafanya kila kitu lakini Shilingi elfu 10,000 ambayo inachukua muda kuipata tunahitaji tuwe na vitu vikubwa lakini tunashindwa” amesema Abdallah.

Mkurugenzi wa uratibu kutoka TASAF, Haika Shayo aliwashauri walengwa wa fedha za TASAF kutumia fedha hizo wanazopata kadiri ya malengo yaliyokusudiwa na kuzingatia maelekezo wanayopewa ili waweze kufika hatua kubwa za kibiashara.

Alipongeza walengwa ambao wamepata mafanikio kupitia Mpango huo kwani wameitendea haki fedha kidogo wanayopoka toka TASAF wamewekeza ruzuku.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Mjini, Salumu Mahida amesema lengo la TASAF ni kuona Wananchi wenye kipato cha chini wananufaika na mpango huo kwa kipato, uwezo lakini pia kujiwekea maendeleo ikiwemo kuboresha Nyumba zao pamoja na kusomesha Watoto wao.

Ujio wa TASAF katika Manispaa hiyo ni kuja kuangalia utekelezaji wa awamu ya tatu kipindi cha pili cha Mpango huo wa Kunusuru Kaya maskini hususani ruzuku ya uzalishaji ambapo Kaya 438 zimenufaika na Mpango ambapo zaidi ya Shilingi milioni 107.

Habari Zifananazo

Back to top button