ELIMU ya ujasilimali na uwekaji wa fedha kupitia vikundi vya kuweka na kukopa kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini imeelezwa kuleta mabadiliko kwa walengwa ambao wameweza kuitumia elimu hiyo kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa ajili ya kuongeza kipato kwa familia.
Hayo yamebainika katika ziara ya kutembelea na kuzungumza na wanufaika wa mpango huo katika halmashauri ya wilaya Kigoma ambao wameeleza kuwa fedha kidogo walizokuwa wakipata wameweza kuzitumia kuanzisha miradi.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo kutoka Kijiji cha Nyabigufa Kata ya Mkongoro halmashauri ya wilaya Kigoma walisema kuwa baada ya kuanza kupokea fedha kutoka TASAF walipewa elimu pia ya ujasilimali na utunzaji fedha kupitia vikundi vya kuweka na kukopa ambapo walianza kukopeshana kuimarisha biashara zao.
Mmoja wa wanufaika hao, Esther Simon alisema kuwa baada ya kuanzaia kupokea fedha katika awamu ya pili ambayo imeendelea hadi awamu hii ya tatu aliwekeza fedha kidogo baada ya kutimiza mahitaji ya msingi akaanzisha biashara ndogo ndogo na baadaye kununua shamba ambalo amenzisha kilimo cha mahindi na maharage.
Naye mohsin Jaffari alisema kuwa baada ya kuwa anapokea fedha kutoka TASAF aliwekeza ili kuanzisha mradi wa kiuchumi baada ya kupata elimu ya ujasiliamali lakini kuelezwa kuwa mpango huo unaweza kufika mwisho hivyo wajiandae kuwa na miradi yao itakayowaingizia kipato.
“Kwa sasa nina shamba la michungwa ambalo lina miti 100 na imeshakuwa na nimeanza kuuza huu ukiwa msimu wa pili, nimeanzisha pia ufugaji wa kuku kwa kuanza na kuku watano na kwa sasa ninao kuku 15, hivyo kwangu naona elimu tuliyopata imetusaidia kuanzisha miradi,”Alisema Mnufaika huyo.