Wanusurika kifo baada ya gari kuteketea kwa moto

WATU watatu wakiwemo wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Bethel Company Limited ya jijini Mwanza wamenusurika kifo baada ya gari waliyokuwa wakisafiria yenye namba T905 DXR, Subaru Foreseter kuteketea kwa moto.

Ajali hiyo imetokea leo Mei 29, 2023 majira ya saa sita mchana katikati ya barabara, eneo la mtaa wa Tambukareli barabara kuu ya Mwanza-Geita mkabala na kituo kikuu cha mabasi mjini Geita.

Dereva wa gari hiyo, Steven Dickson amesema ajali iliwakuta wakiwa safarini kutokea jijini Mwanza kuelekea mjini Geita ambapo ghafla moshi ulianza kufuka ndani ya gari hilo ndipo waliposimamisha gari.

Advertisement

“Gari haikuwa na changamoto yeyote, mara ya mwisho tumekaguliwa Kasamwa (Geita) na askari wa barabarani, tulikuwa vizuri, hii ni gari binafsi ya ofisi.”

Manusura wa ajali hiyo, Rehema Kisaka alisema baada ya moshi kuanza kufuka walishuka na kuomba msaada kwa watu wa karibu na kufanikiwa kushusha mizigo yote ingawa baadhi ya nyaraka zimeteketea.

Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Peter Nkwambi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo taarifa za tukio walipatiwa majira ya saa 6:15 mchana na kufika eneo saa 6:20 mchana.

“Kwa ujuma tumekuta hali ya gari ni mbaya kabisa, inawaka, tumezima huo moto kwa kutumia ‘fomu’ lakini baada ya kufanya upelelezi inaonekana hii gari ilikuwa na watu watatu.” Alifafanua.

Amesema uchunguzi wa awali bado haujabaini chanzo cha ajali hiyo ambapo jeshi la zimamoto litafanya mahojiano na manusura wa ili kupata taarifa zaidi za ajali hiyo.