Wanywaji pombe waongezeka, unywaji kupindukia wapungua

UTAFITI uliofanywa na Kituo cha Matibabu cha Rwanda (RBC) umebaini kuwa kiwango cha watu wanaokunywa pombe nchini kimeongezeka kutoka asilimia 41 mwaka 2013 hadi asilimia 48 mwaka 2022.

Aidha, umebaini kupungua kwa kiwango cha unywaji pombe kupita kiasi kutoka asilimia 23.5 mwaka 2013 hadi asilimia 15.2 mwaka 2022.

Utafiti huo wa hivi karibuni ulilenga kukusanya takwimu kuhusu hatari mbalimbali za magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ulihusisha mahojiano ya ana kwa ana.

Advertisement

Aidha, ulihusisha vipimo vya kimwili na kemikali kutoka kwa watu 5,676 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 69 kutoka mikoa yote minne nchini.

Waziri wa Afya, Dk Sabin Nsanzimana alishirikisha baadhi ya matokeo ya utafiti huo kwenye akaunti yake ya Twitter akisisitiza haja ya watu kubadili mtindo wa maisha ukiwemo unywaji pombe nchini.

Alisema unywaji wa pombe kupita kiasi unasababisha magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za saratani.

“Lazima tubadilike kwa kuepuka pombe na unywaji wa kupita kiasi ili kuishi maisha marefu, yenye afya zaidi na kubaki salama. Pombe si tu ina madhara zaidi kwa vijana, bali pia ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote chini ya miaka 18,” aliandika.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *