WANANCHI wa vijiji vya Lukolongo, Mchombe, Ijia, Mgudeni, Nakaguru na Luvilikila katika kata ya Mchombe halmashauri ya Mlimba , wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro wameiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu katika Mto Mngeta kutokana na lililokuwepo la mbao kusombwa na maji ya mvua.
Walitoa ombi hilo kijijini hapo kufuatia daraja la mbao katika mto huo lililokuwa linaunganisha vijiji hivyo kukatika na kusombwa na maji ya mvua yaliyojaa kwenye Mto Mngeta.
Mkazi wa Kijiji cha Mchombe, Seralina Daudi amesema daraja hilo la mbao lilisombwa na maji tangu Aprili 11, mwaka huu na kuleta adha kubwa kwao kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine .
Hivyo kutokana na adha hiyo, waliiomba serikali kuwajengea daraja imara la chuma litatkalodumu kwa muda mrefu na litakalokuwa ni mkombozi wa kuviunganisha vijiji vyao .
“ Mfano ukiwa na mgonjwa anayehitaji kufikishwa Hospitali upande wa pili wa mto , mgonjwa aliyepungukiwa maji mwilili ama damu inakuwa ni shida kumvusha yeye na wasindikizaji kwa wakati mmoja, “ amesema Seralina.
Naye mkazi wa Kijiji hicho Ridiwani Kilala, amemwomba Rais Dk Samia Suluhu Hassan awatatulie changamoto hiyo kwa kujengewa daraja la kudumu litakalokuwa ni chachu kwao kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo yao ya kiuchumi.
Nao baadhi ya wenyeviti wa vijiji hivyo, akiwemo wa kijiji cha Lukolongo , Aniadi Kateule kwa nyakati tofauti wamesema kuwa kukatika kwa daraja hilo kumesababisha shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi kukwama kwenye vijiji hivyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mchombe , Batholomeo Swalla amemuomba Rais Samia kusaidia uwezeshaji wa kupatikana daraja la chuma litakayokuwa imara .
“ Hapa kuna zaidi ya watu 1,000 wanavuka kila siku kwenye daraja lililokuwepo na baada ya kusombwa na maji kumeathiri shughuli za kijamii na kimaendeleo, “ amesema Swalla