Waomba mchakato kuwaondoa Ngorongoro uharakishwe

Waomba mchakato kuwaondoa Ngorongoro uharakishwe

WAKAZI wanaoishi katika Kijiji cha Kapenjiro, kata ya Naiyobi, Tarafa ya Ngorongoro na wengine waliopo ndani ya  Hifadhi ya Ngorongoro, wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa kuwaondoa eneo hilo ili waweze kuendeleza maisha yao kwenye maeneo mengine waliyojiandikisha ikiwemo Msomera.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Kapenjiro wilayani Ngorongoro,wananchi hao wakiongozwa na  Ndwala Ngoishiye , Petro Tengesi wamesema maisha katika eneo hilo hayafanani na maisha halisi ya mwanadamu.

Advertisement

Ngoishiye amesema wapo tayari hata leo waondoke eneo hilo, kwani wanakosa huduma muhimu za jamii, ikiwemo mawasiliano ya simu, na hata mgonjwa akiumwa wanambeba kwa machela hadi Engaruka na kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 100, kwani wanatembea zaidi ya saa15 kutafuta huduma za afya.

Amesema kaya zaidi ya 70 zenye watu zaidi ya 140, zinasubiri kuondoka na waliotangulia wamefika Msomera na kupata huduma muhimu za kijamii, lakini wanaoendelea kukaa Ngorongoro wanaishi kinyonge na hata kama nyumba bado wapo tayari kuondoka na kwenda Msomera kujenga wenyewe nyumba zao, ili waondoke eneo hilo.

Naye Elizabeth Petro ameomba suala hilo lifanyike haraka, ili watoto waweze kusoma kwa raha huko watakakoenda.