WAMILIKI wa mabasi nchini, wameiomba serikali kupunguza ushuru wa kuingiza mabasi ambao umepanda kutoka Sh milioni 40 hadi milioni 90.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa ofisi za spea za Yutong, wamemiliki hao wamesema kuwa ushuru unaotozwa na serikali ni mkubwa, kiasi kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanashindwa kumudu.
Muhsin Said, mwakilishi wa mabasi ya Shabiby ameema: “Serikali iangalie namna ya kupunguza ushuru, ushuru umekuwa mkubwa sana kwa basi moja kuingiza imefika sh milioni 90, ndio maana watu wengi wanashindwa kumudu na kupotea katika soko.”
Naye mmiliki wa mabasi ya Lupundije Express, Rogers Malaki, amesema vipengele vingi kwa wawekezaji ni kikwazo.
“Wenzetu wanavyokuja kuwekeza wanategemea kukutana na mazingira rafiki ya uwekezaji wanapokutana na vikwazo kidogo inakuwa tabu na wengine wanashindwa na kuondoka,”amesema.
Msimamizi wa mabasi ya Ester, Godwin Saul kwa upande wake alizungumzia ufunguzi wa ofisi ya Youtong nchini kuwa utakuwa na manufaa makubwa, kwanza utasaidia kuwa na uhakika wa spea na zitapatikana kwa urahisi tofuati na ilivyo sasa.
Kwa upande wa mwakilishi wa Yutong Tanzania, Erick Si amesema kiwanda hicho kitakuwa kikubwa na kitahudumu nchi zote za Afrika Mashariki na Kati.
Amesema hiyo itatoa fursa kwa wafanyabiashara wa magari kuwa na uhakika wa kupata spea halisi na bora kwa gharama nafuu tofauti na sasa.
Amesema, Yutong zenye injini mbele ziliingia soko la Tanzania kwa mara ya kwanza 2009/10 na hadi sasa mabasi zaidi ya 500 yapo kwenye soko la Afrika Mashariki.
“Yutong ni kampuni kubwa duniani ya utengenezaji mabasi, 2015 tuliuza magari 67,000 duniani yenye thamani ya Dola 4 bilioni za Marekani na kuwa kampuni pekee ambayo mauzo yake yanakua kwa asilimia tisa kwa mwaka,” amesema Si.
Comments are closed.