Waombaji wasio na sifa ya ukimbizi kurudishwa

Waombaji wasio na sifa ya ukimbizi kurudishwa

SERIKALI ya Tanzania imesema haitawapa hifadhi ya ukimbizi, waomba hifadhi kutoka nje ya nchi ambao hawana sifa ya ukimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kupokea na kuhifadhi wakimbizi pamoja na sheria za nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ametoa kauli hiyo ya serikali alipotembelea na kukagua vituo vya muda mjini Kigoma vinavyotumika kuwapokea na kuwafanyia mahojiano ya awali waomba hifadhi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ili kuwapa hadhi ya ukimbizi.

Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mjini Kigoma akihitimisha ziara yake ya siku moja kutembelea vituo hivyo, alisema taarifa alizoletewa na wasaidizi wake na mahojiano aliyofanya na baadhi ya wakimbizi amebaini idadi kubwa ya waomba hifadhi hao hawana sifa ya kupata hadhi ya ukimbizi.

Advertisement

Alisema kuwa wengi wa waomba hifadhi hao hawakuingia mkoani Kigoma moja kwa moja, kulingana na taratibu za kimataifa za kupokea na kuhifadhi  wakimbizi na sheria za nchi na mahojiano mengi yanabainisha kuwa wengi wa waomba hifadhi hao wamekimbia matatizo ya kiuchumi kwenye familia zao na kwamba hizo siyo sababu zinazoweza kuwapa hadhi ya ukimbizi.

Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni (katikati), akipata taarifa za namna waomba hifadhi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC),wanavyopolelewa na kufanyiwa mahojiano ya awali. (Picha zote na Fadhil Abdallah).

“Nimefanya mahojiano na baadhi ya waomba hifadhi na kwa masikio yangu wameniambia kwamba baadhi yao wamekuja baada ya kusikia wenzao wanakuja Tanzania, kwa sababu sasa hivi wakimbizi wapya wanapokelewa na hao walikuwa wakiishi maisha yao ya kawaida nchini DRC.

“Mwingine alisema kuwa amekuja kuomba hifadhi ya ukimbizi kwa sababu mume wake amemkimbia na watoto, hivyo ana hali ngumu ya maisha,” alisema Waziri Masauni.

Katika kuhakikisha sheria za kimataifa za kupokea wakimbizi na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, ametoa maelekezo kwa watendaji wa idara ya wakimbizi, UNHCR na vyombo vya ulinzi na usalama kuwapokea, kuwahoji na kujiridhisha na taarifa za waomba hifadhi hao na wale ambao hawana sifa warejeshe nchini mwao, kwa makubaliano ya pande zote.

Alisema kuwa uwepo wa waomba hifadhi unahusiana kwa karibu na hali ya ulinzi na usalama wa nchi na kwamba kama waomba hifadhi hao hawana matatizo ya kiusalama kwenye maeneo yao, inatia shaka kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini, hivyo kunahitajika umakini katika kusimamia jambo hilo.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi, Sudi Mwakisi alisema kuwa hadi kufikia jana jumla ya waomba hifadhi 7645 wamepokelewa katika vituo vya Buhabugali na ofisi za idara ya wakimbizi Kanda ya Magharibi na kufanyiwa mahojiano ya awali na kati yao waomba hifadhi 5465 wamepelekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, akiwahoji baadhi ya wakimbizi wa DRC.

Mwakibasi alisema kuwa waomba hifadhi hao wamepelekwa kambini Nyarugusu wakisubiri kujua hatima yao kutoka kamati ya Taifa inayoshughulikia kutoa hadhi ya ukimbizi, lakini takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya waomba hifadhi waliohojiwa hawana sifa ya ukimbizi zaidi ya kuwa na matatizo ya kiuchumi.

Akiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye, Waziri Masauni amemtaka Mkuu huyo wa mkoa na Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kutekeleza majukumu yake kikamilifu katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa mkoa na kuzuia wageni kuingia mkoani humo kiholela.

Akizungumza mbele ya Waziri wa mambo ya ndani,  Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye, alisema kuwa wanachukua hatua zote muhimu za kusimamia ulinzi na usalama wa mkoa na kupokea maelekezo ya kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini kupitia mkoani humo wanatambulika hadhi zao na taarifa zao muhimu za mahali walipotoka kwa ajili ya usalama wa mkoa huo.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *