Waonya matumizi holela dawa za kulainisha choo

WATAALAM wa afya wameonya matumizi holela ya dawa za ‘laxactive’ kwa ajili ya kulainisha choo, wakasema ni mojawapo ya chanzo cha kuathiri mfumo wa chakula.

Zinapotumika bila maelekezo ya mtaalam, zinalazimisha maji kukusanyika katika matumbo kwa dharura, kutoka kila pembe ya mwili ili kusaidia kulainisha choo, hatimaye kumfanya mgonjwa aharishe.

“Kuharisha kwa kasi ndiko kunakoathiri mfumo wa chakula,” amesema muuguzi msaidizi hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Paschael John.

Ameelimisha zaidi kwamba mfumo mmoja katika mwili wa binadamu unapoathirika, mingine yote inavurugika na kusababisha matatizo kiafya.

Mfano amesema, dharura ya kukusanyika kwa maji katika matumbo inasababisha sehemu zingine za mwili, ikiwemo figo, kupungukiwa maji na hivyo kusababisha uwepo wa mawe kwenye figo.

Pia amesema maji yatapungua katika mfumo wa kutoa taka mwili nje, hali inayosababisha mkojo kubadilika rangi na kuwa wa njano, huku ukitoa harufu kali.

Amesitiza mwenye matatizo ya choo kigumu kuwasiliana na wataalam, kwani zipo njia za asili za kutatua changamoto hiyo bila kutumia dawa.

Mojawapo ya njia asili ni kutokula chakula kigumu na kikavu, pamoja na kunywa maji ya kutosha, si chini ya lita mbili kwa siku (saa 24) au lita 1.5 kwa saa 12.

“Lakini pia kila mlo uwe na mbogamboga pamoja na matunda ya kutosha, ili kurahisisha mmeng’enyo na hivyo kulinda mfumo mzima wa chakula,” ameelimisha.

Wataalam pia wameshauri kutokula chakula na kunywa maji kwa wakati mmoja, kwa sababu maji yanapenya haraka kwenye matumbo na kuzuia mmeng’enyo wa chakula.

Maji yanyweke nusu saa baada ya chakula, na kwa yule mwenye hofu ya kukabwa (na chakula) atumie matunda yenye asili ya maji, kama vile matikiti maji na matango.

Imeshauriwa zaidi kwamba mitindo hatarishi ya maisha pia iepukwe, kwani ni moja ya chanzo cha kuathiri mfumo wa chakula, kupitia hasa unywaji pombe uliokithiri pamoja na ulaji wa vyakula vyenye asidi/vichachu.

Vyakula hivyo na pombe vinapoingia tumboni hukwangua ute uliopo kwenye kuta za matumbo, ambao kazi yake ni kusaidia chakula kuteleza na kuelekea kunakostahili mwilini.

Kadahalika ulaji wa vyakula vichachu uliopitiliza huathiri asidi asili anayozaliwa nayo binadamu katika matumbo, ambayo kazi yake pia ni kusaidia mmeng’enyo na vilevile kuua bakteria wanaoingia tumboni, hasa pale kunawa mikono kabla ya kula au kuosha chakula kunaposahaulika.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button