Waonywa matumizi dawa kuongeza nguvu za kiume

KAIMU Mkurugenzi Udhibiti wa Dawa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk Yonah Mwalwisi amesema miongoni mwa madhara ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kiholela ni kusababisha maumivu makali sehemu za siri.

Amesema hali hiyo isipodhibitiwa kwa haraka inaweza kuharibu mishipa laini iliyoko ndani ya sehemu hizo na kusababisha tatizo kubwa zaidi.

Akizungumza na HabariLEO katika mahojiano maalum Dk Mwalwisi amesema madhara mengine ni kuwa zikitumika sambamba na dawa zinazotibu maumivu ya moyo, husababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa shinikizo la damu, kupata kizunguzungu, kuzimia, mshtuko wa moyo, kiharusi na mengine ambayo husababisha kifo.

Kwa mujibu wa Dk Mwalwisi, mwanaume aliyegundulika kitaalamu kuwa na tatizo hilo na daktari atamchagulia aina ya dawa na kumuelekeza matumizi sahihi ya dawa hiyo.

Amesema kwa kawaida dawa hizo huchukua takribani dakika thelathini ili kuanza kufanya kazi kama hakuna vikwazo vya mwili au mwingiliano na dawa zingine.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kitaalamu dawa hizo zina muda maalumu wa kuzitumia na wengi hupewa saa moja kabla hajakutana na mwenza wake.

“Haishauriwi kabisa kutumia dawa hizi zaidi ya mara moja kwa siku na ni muhimu kuwasiliana na mtaalamu wa afya kama kuna umuhimu wa kukuchagulia dawa yenye kufanya kazi kwa muda mrefu mfano ili kuepuka matumizi ya mara kwa mara ya dawa,” amesema Dk Mwalwisi.

Kwa mujibu wa Dk Mwalwisi, dawa hizo hazitafanya kazi moja kwa moja au vizuri endapo tatizo hilo la kupungukiwa na nguvu za kiume linatokana na kuathirika kisaikolojia.

“Mfano kutokuwa na hamu ya kufanya mapenzi, kutokujiamini, woga au kuwa na hofu ya kimapenzi na mwenza wako Tafiti zimeonesha kuwa dawa hizi hazitibu kabisa hayo na haziongezi hamu au shauku ya kufanya mapenzi,” amesema.

Amesema mhusika mwenye tatizo anapaswa kumwona daktari ili afanyiwe uchunguzi wa chanzo cha tatizo, ukubwa wake na kupewa aina ya dawa na matumizi sahihi.

Dk Mwalwisi amesema dawa zinazotumika kutibu tatizo hilo zipo kwenye kundi linaloitwa phosphodiesterase type 5 (PDE5) inhibitors ambazo husababisha mzunguko wa damu kuwa mzuri ndani ya mishipa ya sehemu za siri za mwanaume.

“Mifano ya dawa hizi ni Sildenafil, Tadalafil, Vardenafil na Avanafili na kati ya dawa hizi nne, tatu zimesajiliwa na TMDA na zina majina tofauti tofauti kama vile Sindenafil majina mengine ni Evoke, Erecto, Zwagra, Silment, Njoi na Viagra, nyingine ni Tadalafil (Saheal na Cialis) na Vardenafil (Levitra).

Amebainisha kuwa upungufu wa nguvu za kiume husababishwa na vyanzo mbalimbali mfano kunywa pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, ukubwa wa mwili, uvutaji wa sigara au dawa za kulevya, msongo wa mawazo, kuwa na vichocheo vichache na aina ya vyakula.

Dk Mwalwisi amesema kama tatizo linasababishwa na hayo aliyoeleza hapo juu linaweza kupona au kupungua kwa kiasi kikubwa endapo atafuata ushauri wa daktari na kuacha yaliyoelezwa hapo juu.

“Kama chanzo ni upungufu wa hormones za kiume, basi matibabu ya aina hiyo yatahitajika, kuacha kutumia dawa nyingine ambazo husababisha tatizo hili, kupunguza uzito, kufanya mazoezi pamoja na kubadilisha hali ya kuishi ambayo ilikusababishia tatizo hilo pia zinaweza kusaidia kutibu kabisa tatizo hili.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button