SHIRIKA la kimataifa la World Organisation For Science Literecy lenye makao makuu yake Beijing, China limefungua kituo cha mafunzo mkoani Geita, ili kuongeza uelewa na ufaulu masomo ya sayansi.
Mwakilishi wa shirika hilo, Stephen Kamunya amebainisha hayo mbele ya waandishi wa habari katika mahafali ya shule ya awali na msingi Kadama, ambayo ndio kituo teule cha shirika hilo mkoani Geita.
Kamunya ambaye ni muhitimu wa chuo kikuu cha Autsralia, amesema kwa Kanda ya Ziwa kituo kikuu cha Sayansi kipo Pasiansi mkoani Mwanza, dhamira ikiwa ni kufundisha sayansi kwa kutumia zana rahisi.
“Lengo letu ni kutibu changamoto inayokuwepo kwenye mashule kwa ukanda wa Afrika, kwani nchi zetu zina upungufu wa maabara, lakini kama utakuta kuna maabara utakuta vifaa havitoshelezi,” amesema.
Amesema mpaka sasa shirika limezifikia shule 305 Tanzania Bara na Zanzibar, huku kwa Kancda ya ziwa wamefika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu na kwa sasa watawekeza mkoani Geita.
“Kati ya shule hizo 305, kwa upande wa Geita tumeweza kufika Kadama English Medium na tumeona ni sehemu sahihi sisi kwetu kuwekeza nguvu yetu kwa kushirikiana na shule hii, ili kufikia malengo.
“Baadhi ya shule tumeshajenga vituo vya kufundishia, hizo shule 305 tumezifikia kupitia maabara inayotembea, tunatumia vifaa vya kawaida na vifaa vya kisasa, tunatoa semina kwa walimu na watoto.”
Mkurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Kadama English Medium iliyopo Chato Geita, Leticia Pastory ameeleza mwamko na ufaulu mzuri wa masomo ya sayansi kwenye shule ndiyo umevutia shirika hilo kufungua kituo shuleni hapo.
“Kwa hiyo na sisi tumewapa ushirikiano, kwa sababu tunahitaji idadi ya watoto wetu wanaosoma sayansi iongezeke, kama tunavyojua dunia ya leo ni sayansi na teknolojia,” amesema Leticia.