Wapatiwa mizinga kuongeza uzalisha asali

VIKUNDI zaidi ya vitano vya ufugaji nyuki kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi wa Barrick Bulyanhulu uliopo Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepatiwa mizinga zaidi ya 200 na kupewa mafunzo ya namna ya kuchakata asali ili waweze kuingia kwenye ushindani wa soko la asali.

Kaimu meneja Mahusiano ya jamii na Mazingira kutoka kwenye mgodi huo, Zuwena Senkondo aliyasema hayo juzi walipotembelea wafugaji wa kikundi cha Kwikondele kilichopo kijiji Cha Buyange kata ya Bugarama.

Senkondo alisema vikundi hivyo vimekuwa vikiwezeshwa kutembelea maonyesho mbalimbali ya bidhaa ili kujifunza namna kutafuta masoko na kila jumamosi kumekuwa na darasa la wajasiriamali linaloitwa biashara yako biashara yangu.

Advertisement

“Tumejenga kituo cha kuchakata asali na kina vifaa na mitambo yote ili vikundi hivyo viweze kutumia kituo hicho kuchakata nakupata asali nzuri yenye viwango vinavyo hitajika katika soko” alisema Senkondo.

Katibu wa kikundi cha kwikondele Samson Mbonde alisema Mgodi umewawezesha mizinga ya nyuki 17 mwaka 2015 ndiyo walianza mradi huo na waliweza kuvuna Lita kumi kwenye mzinga mmoja hali ikiwa mbaya lakini wanauwezo wakuvuna Lita zaidi ya kumi kulingana na hali ya hewa.

“Kikundi hiki kina wanachama 13 Tumeweza kufungua akaunti benk nakutunza sh 600,000 lakini Sh milioni 1.5 tumekopeshana baada ya kuuza asali na asali na dumu la Lita 20 moja tulikuwa tunauza kwa sh 180,000.”alisema Mbonde.

Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho Bertha Nyawaga alisema kupitia ufugaji nyuki amenufaika kupata somo la ufugaji ambalo amekuwa akifundishwa ametembelea Masoko ya nje ya mkoa kujifunza zaidi,amenunua shamba nakusomesha watoto wake.

Diwani wa kata ya Bugarama Prisca Musoma alisema kupitia Fedha za huduma kwa jamii (CSR) Mgodi huo umewezesha makundi mbalimbali ya ujasiriamali upande wa vikundi vya ufugaji nyuki wajasiriamali kwanza wamepata elimu na kuongeza kipato kwenye Kaya zao ukiachana na Ile asilimia kumi inayotolewa na halmashauri.

Ofisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya Msalala Judica Sumari alisema amekuwa mwezeshaji katika darasa la wajasiriamali wadogo na kila kipindi wanahudhuria wajasiriamali wasiopungua 80 walio wengi wamekidhi vigezo nakuweza kurasimisha bidhaa zao nje na ndani ya nchi..