Wapendekeza sheria ya ugaidi ipitiwe upya

CHAMA cha Wanasheria nchini (TLS) kimependekeza kuboreshwa na kupitiwa upya  sheria ya ugaidi kwa sababu sheria hiyo haisemi nini maana ya ugaidi.

Pia wamesema sheria hiyo ina changamoto kwa sababu ilichukuliwa kutoka nchi za jirani, hivyo kuna umuhimu wa kurekebisha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Wakili na Mjumbe wa Kamati ya TLS, Frank Mchomvu baada ya kutoa mapendekezo kwa Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai Nchini, alisema sheria ya ugaidi haijaainisha ni makosa gani mtu akifanya ndio anakuwa amefanya ugaidi.

“Sheria ya ugaidi haijasema ugaidi ni nini, hivyo ingepitiwa na kuboreshwa ndio maana  inaweza kuleta changamoto kwa sababu ni miongoni mwa makosa yasiyokuwa na dhamana na sheria hii ilitoka nje kutokana na msukumo ulikuwepo kipindi kile, inawezekana kile ambacho ni ugaidi kwa Marekeni, Tanzania isiwe ni ugaidi,” alisema Mchomvu.

Alipendekeza kuboresha taasisi zinazohusika na haki jinai kama vile polisi, ofisi ya taifa ya mashitaka mahakama kama wadau na mapendekezo ya sheria moja kwa moja na baadhi ya vifungu viwekwe pamoja kwa lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini.

Akitolea mfano Kifungu cha 36 cha sheria ya makosa ya uhujumu uchumi na uharifu wa  kupanga, alisema  kifungu hicho kinatoa mamlaka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kuweka haki ya kuzuia kutoa dhamana kwa mtuhumiwa.

Mchomvu alisema pia katika sheria ya utakatishaji wa fedha haramu kwakuwa kuna kifungu kinazipa mamlaka na taasisi kumuadhibu mtu ambaye hajazingatia matakwa ya sheria,  kwa hiyo wamependekeza hicho kifungu kiboreshwe ili  kama mtu anakuwa hajatimiza  sheria aadhibiwe na mahakama na sio taasisi nyingine.

Alisema wametoa pendekezo kwa mahakama inayohusu makosa ya rushwa na uhujumu uchumi iwe ni division ya makosa ya jinai kwa ujumla, isiwe tu inashughulika na makosa ya uhujumu uchumi na rushwa kwa sababu mashauri ya jinai yanaenda kwa muda mrefu na mtuhumiwa anakuwa ndani kwa muda mrefu.

Habari Zifananazo

Back to top button