Wapewa maelekezo matumizi Bandari ya Karema 

MAANDALIZI ya kuanza kutumika kwa Bandari ya Karema, iliyopo wilayani Tanganyika, Mkoa Katavi yamekamilika kwa asilimia 100.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Onesmo Buswelu, amewataka wadau, wafanyabiashara na wote wanaotarajia kutumia Bandari ya Karema kuwa wazalendo, kwa kuchangia stahiki zote za serikali zilizopo kisheria.

Ameyasema hayo katika kikao kazi na wadau wa Bandari hiyo kilichofanyika jana, alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ambapo amesema uwepo wa bandari hiyo unalenga wawekezaji kufanya kazi mazingira salama.

Bandari hiyo iliyopo Kata na Tarafa ya Karema Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, inatarajia kuanza kazi kesho Alhamisi, Septemba mosi na  imeelezwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100.

“Ni fahari kwa Mkoa wa Katavi kuwa na bandari kubwa na ya kisasa, hivyo nawaomba wafanyabiashara kuacha kutumia bandari bubu, badala yake waitumie bandari hiyo kwa ajili ya usalama wa mizigo yenu, ikiwemo kuongeza mapato ya mkoa na nchi kwa ujumla,”alisema Buswelu.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ukanda wa Ziwa Tanganyika, Edward Mabula amesema bandari hiyo inatarajia kutoa ajira kwa wananchi wapatao 1,500, pamoja na kutoa fursa mbalimbali za kibiashara, zikiwemo za makazi kutokana na eneo hilo kutokuwa na makazi ya kutosha.

Habari Zifananazo

Back to top button