MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege nchini, imekabidhi mifuko ya saruji yenye thamani ya Sh milioni 5 kwa uongozi Kijiji cha Majalila, kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi ya Inyagantambo, iliyopo Kata ya Tongwe, Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Meneja Uwanja wa Ndege Mpanda, Jeff Shantiwa amesema, wameguswa kuchangia baada ya kupata maombi na kusikia kuwa watoto wanaoishi kitongoji cha Inyagantambo, wanatembea umbali wa kilomita 28, kwa siku kwenda kupata masomo shule ya Msingi Mpandandogo, iliyopo Kijiji cha Majalila.
“Kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, tuna sera ya kurudisha kwa jamii, hivyo lengo la kuchangia mifuko 237 ya saruji ni kusapoti ujenzi wa Shule ya Msingi Inyagantambo na kusaidia watoto wa kitongoji hicho kutotembea, umbali mrefu kufuata elimu,” amesema Shantiwa.
Naye Diwani wa Kata ya Tongwe, Frank Mibigasi ameishukuru mamlaka hiyo, kwa kuwa wadau wakubwa katika shughuli za kijamii, hasa miradi ya maendeleo na kuahidi kuwa mifuko hiyo ya saruji itafanya kazi iliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila, Ally Mashaka, amesema Shule ya Msingi Mpandandogo, ina jumla ya wanafunzi 1,400, ambapo kati yao wanafunzi 150, wanatoka kitongoji cha Inyagantambo, hivyo kusababisha msongamano wa wanafunzi katika shule hiyo.
“Tuna uhitaji wa vyumba vya madarasa 36, lakini kwa sasa tuna madarasa 14, hivyo tuna upungufu wa madarasa 22, jitihada ambazo tunazifanya, ili kupunguza changamoto, hiyo tumeamua kuanzisha shule nyingine katika Kitongoji cha Inyagantambo,” amesema Mashaka.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mpandandogo, Halima Naison, amesema mbali na kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu, lakini pia ujenzi wa shule hiyo shikizi utasaidia weledi wa wanafunzi darasani, kwani wengi hulazimika kushinda na njaa kutokana na kuishi mbali na maeneo ya shuleni.
Umbali kutoka Kitongoji cha Inyagantambo hadi Kijiji cha Majalila ni kimolita 14, ambazo kwenda na kurudi hufika kilomita 28.