Wapewa msaada wa magari programu za elimu

WIZARA  ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea magari mawili yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 250 kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Uingereza la UK-AID kwa ajili ya ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za kielimu za Program ya shule bora nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika  leo Novemba 16, 2023 katika Ofisi za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)  jijini Dar es Salaam na kupokelewa na  Naibu Katibu  Mkuu wa WyEST, Franklin Rwezimula na  kuyakabidhi kwa Naibu Katibu OR -TAMISEMI Dk  Charles Msonde tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk Rwezimula  ameishukuru UK-AID kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha Sekta ya Elimu kwa kutoa magari hayo yatayosaidia utekelezaji wa mradi huo.

Advertisement

“Tunashukuru kwa msaada huu, kwani utaimarisha ufuatiliaji  na tathimini katika miradi ya elimu  na umekuja wakati muafaka  kujua  utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini changamoto mbalimbali,” amesema Dk  Rwezimula.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, OR-TAMISEMI Dk Charles Msonde amesema  TAMISEMI kama watendaji katika ngazi za mikoa na serikali za mitaa wataendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika yanayoendelea kusaidia katika kuboresha masuala mbalimbali ikiwemo elimu nchini.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo wa Ubalozi wa Uingereza hapa nchini, Kemi Williams ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano walionesha katika kuhakisha magari hayo yananunuliwa ili kwenda kusaidia katika utekelezaji wa Programu ya Shule Bora utakaosaidia maboresho katika Sekta ya elimu nchini kupitia ufuatiliaji na tamthimini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk  Aneth Komba amesema TET kama watekelezaji wa mradi wa shule bora kupitia mafunzo tayari, imetoa mafunzo kwa walimu na viongozi mbalimbali wa elimu  nchini yakiwemo ya mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zinazozingatia ujumuishi wa walimu.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *