Wapewa siku 14 watenge maeneo ya malisho, kilimo
SINGIDA; Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ametoa siku 14 kwa viongozi wa Vijiji vya Damwelu, Doroto na Itigi Halmashauri ya Itigi mkoani Singida kuwa kila kijiji kutenga maeneo ya malisho na kilimo, ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Ametoa mda huo baada ya kutatua mgogoro kati ya wafugaji na wakulima katika vijiji hivyo uliodumu kwa zaidi ya miaka 12, kutokana na baadhi ya wakazi hao kuanza kuvamia na kulima maeneo yaliyotengwa kwa umoja wa vijiji hivyo kwa ajili ya ufugaji.
Baada ya kuwasikiliza wananchi, Serukamba alitoa maelekezo kwa kuwaagiza viongozi wa vijiji hivyo kuwa kila kijiji kutenga maeneo yake ya ufugaji na kilimo.
Hofu kwa wakazi hao ni kudai kuwa kuna baadhi ya maeneo katika vijiji vyao yameuzwa na baadhi ya viongozi,hivyo hawana uhakika kama watapata maeneo hayo ya kilimo na ufugaji.
Amewatoa hofu wananchi, ambapo amesema kama kuna viongozi wameshiriki kuuza maeneo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.
Vijiji vya Damwelu, Doroto na Itigi katika Halmashauri ya Itigi viliungana kwa pamoja na kutenga eneo moja la malisho na kilimo, lakini umoja huo ulishindikana na kufanya mgogoro mkubwa kwa wakazi wa vijiji hivyo.